Mabasi yarejelea safari zao za usiku, serikali ikijikokota kutoa mwongozo

Mabasi yarejelea safari zao za usiku, serikali ikijikokota kutoa mwongozo

WANDERI KAMAU na KIPKOECH CHEPKWONY

WAKENYA bado wamechanganyikiwa kuhusu ikiwa wanapaswa kurejelea biashara zao huku kampuni za mabasi ya masafa marefu yakianza safari za usiku.

Wakenya wengi waliozungumza na Taifa Leo walisema bado wamo gizani, kwani serikali haikutoa ufafanuzi kamili kuhusu masharti mapya.

Wale wanaoeleza kuchanganywa na tangazo la Rais Uhuru Kenyatta ni wafanyabiashara wadogo hasa katika maeneo ya mijini.

Madereva wa magari ya masafa marefu pia wanalalamika kuachwa gizani, kwani hawajui ikiwa hatua ya Rais inawaruhusu kurejelea safari za usiku.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, jana Alhamisi alisema kuwa, wizara za Uchukuzi na Michezo zitatoa mwongozo kuhusu masharti yatakayoendelea kuzingatiwa ili kuondoa suitafahamu iliyopo.

Hata hivyo, wadau katika sekta ya uchukuzi walisema wizara husika inapaswa kuharakisha kutoa mwongozo huo, ili kuwaruhusu kurejelea shughuli zao kikamilifu kama ilivyokuwa awali.

Alhamisi, kampuni ya mabasi ya Modern Coast Express Ltd ilitangaza kuanza safari zake za usiku kati ya Mombasa na Nairobi.

“Tunawatangazia kuwa kuanzia leo (jana Alhamisi) tunaanza safari za usiku na abiria wote wanahitajika kuwasili dakika 30 kabla ya muda wa kuondoka,” ikasema kampuni hiyo.

Nayo kampuni ya Ena Coach ilisema imerejelea safari zake za usiku kuanzia leo, kati ya Mombasa na magharibi mwa Kenya.

Kampuni ya Easy Coach, jana Alhamisi pia ilitangaza kuwa imerejelea safari za usiku kama kawaida, na kuhimiza wateja wake kuanza kukata tiketi.

Bw Kagwe alisema hoteli na vituo vya burudani vitakuwa vikifungwa saa tano za usiku.

Akihutubu kuhusu hali ya virusi vya corona nchini, Bw Kagwe alisema mikahawa na maeneo ya burudani yataendelea kuzingatia baadhi ya masharti kama ambavyo imekuwa awali.

“Hoteli na maeneo ya burudani zitahitajika kuendelea kuweka maeneo ya wateja kunawa mikono na kuhakikisha kwamba hawakaribiani,” akaeleza Bw Kagwe.

Wafanyabiashara wadogowadogo katika mitaa kadhaa viungani mwa Nairobi walilalamika kuendelea kuhangaishwa na polisi, kwani serikali haijaweka wazi ikiwa wako huru kuendesha shughuli zao kwa muda wa saa 24.

“Ikiwa serikali itatoa mwongozo ufaao, basi tutakuwa huru kuendesha biashara zetu bila wasiwasi wowote. Hata hivyo, kuna hali ya suitafahamu hadi sasa,” akasema Bi Mary Khayesi, ambaye ni mchuuzi katika mtaa wa Umoja, Nairobi.

Malalamishi kama hayo pia yametolewa na baadhi ya wahudumu wa bodaboda, ambapo walisema “serikali itawaharibia pato” ikiwa hoteli na vituo vya burudani vitafungwa saa tano usiku.

You can share this post!

AU yaunga Mkenya kujiunga na tume ya UN

Rais apewa siku 14 na mahakama kuapisha majaji 6

T L