Habari Mseto

Mabaunsa wafikishwa kortini kushtakiwa

January 10th, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MABAUNSA waliokamatwa pindi baada ya shambulio dhidi ya wanahabari mnamo Januari 5, 2024, katika kilabu kinachofahamika kama Kettle House Bar, Kileleshwa, wamefikishwa katika Mahakama ya Milimani kushtakiwa.

Soma Pia: MCK yalaani shambulio dhidi ya wanahabari jijini Nairobi

Wanahabari walishambuliwa Ijumaa walipokuwa wakinakili matukio wakati wa operesheni kali ya Mamlaka ya Kitaifa ya Kampeni Dhidi ya Pombe na Mihadarati (Nacada) katika kilabu hicho.

Operesheni hiyo iliongozwa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Nacada, Bw Anthony Omerikwa.

Watu kadhaa walipatikana wakivuta shisha.

Mabaunsa ambao hawakutaka vyombo vya habari vianike uovu huo, waliwajeruhi wanahabari kwa visu na silaha butu.

Baraza la Vyombo vya Habari Nchini (MCK) lililaani vikali shambulio hilo, likilitaja kama uingiliaji wa haki ya wanahabari kutekeleza majukumu yao.

“Kwa kuwalenga wanahabari ambao walikuwa wakitekeleza majukumu yao, lengo kuu la washambuliaji hao lilikuwa kuvizuia vyombo vya habari kutekeleza jukumu lake la kuwafahamisha Wakenya kuhusu masuala yanayohusu maisha yao,” likaeleza baraza hilo kwenye taarifa.