Habari

Mabilionea nchini waongezeka licha ya serikali kulia haina hela

March 8th, 2018 1 min read

Na VALENTINE OBARA

IDADI ya mabilionea nchini iliongezeka mwaka 2017 licha ya serikali, wafanyabiashara na wananchi wengi kuzidi kulalamika kuwa kipindi kirefu cha kisiasa na kiangazi zilisababisha hali ngumu ya maisha.

Ripoti ya Utajiri Ulimwenguni iliyotolewa Jumatano usiku na shirika la Knight Frank inaonyesha kuna Wakenya 100 ambao kwa jumla wana utajiri wa Sh964 bilioni, kiwango ambacho ni sawa na karibu nusu ya bajeti ya taifa.

Makadirio ya bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2018/2019 yaliyochapishwa Januari 2018 yanaonyesha serikali imepanga kutumia Sh2.2 trilioni.

Kulingana na ripoti hiyo, kuna Wakenya kumi wenye utajiri wa dola 500 milioni (Sh50.5 bilioni) kila mmoja. Hii ni kumaanisha kuwa kwa jumla wakwasi hao ambao hawakufichuliwa wana utajiri wa Sh505 bilioni.

Mbali na hayo, idadi ya Wakenya wenye utajiri wa Sh5.1 bilioni kila mmoja iliongezeka kutoka watu 80 katika mwaka wa 2016 hadi 90 mwaka 2017.

Vile vile, wananchi ambao utajiri wao ni Sh505 milioni kila mmoja waliongezeka hadi watu 1,290 mwaka uliopita kutoka watu 1,110 mwaka wa 2016.

Watafiti walihoji washauri wa uwekezaji katika mashirika ya kifedha nchini ambao walisema inatarajiwa idadi ya wakwasi itazidi kuongezeka katika miaka ijayo.

Ilibainika wengi walipata utajiri kutoka kwa uwekezaji katika sekta ya ujenzi, fedha, viwanda na uuzaji wa bidhaa za nyumbani.

Ripoti hiyo ilitolewa wakati ambapo serikali imetangaza kufilisika na hivyo basi kuleta wasiwasi kuhusu hatima ya wananchi kwani inatarajiwa hali hiyo itaathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.

Imetolewa pia wakati ambapo kampuni mbalimbali zinazidi kuweka mikakati ya kupunguza gharama za matumizi ya fedha hasa kwa kupunguza idadi ya wafanyakazi kutokana na upungufu wa faida.

Zaidi ya hayo, ripoti hiyo imeonyesha pengo kubwa la kimaisha lililopo kati ya mamilioni ya wananchi wachochole na mabwanyenye wachache.

Mwezi uliopita, Katibu Mkuu wa Shirika la Kenya Red Cross, Bw Abbas Gullet, aliomba Sh1 bilioni ili kusaidia wananchi karibu milioni 3.4 wanaokumbwa na janga la njaa katika pembe tofauti za nchi.