Mabilioni ya miradi ya serikali ndiyo ‘hutafunwa’ zaidi – Ripoti

Mabilioni ya miradi ya serikali ndiyo ‘hutafunwa’ zaidi – Ripoti

Na PETER MBURU

MIRADI inayofadhiliwa na fedha za walipa ushuru ndiyo inayotafunwa zaidi na maafisa fisadi serikalini, ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imefichua.

Hili ni kinyume na miradi inayoendeshwa na wafadhili, kwani fedha zinazotumika huwa zinasimamiwa kwa njia nzuri.

Usimamizi mzuri wa miradi hiyo huwa unazima nafasi ya fedha hizo kuporwa. Hilo pia limeifanya miradi hiyo kuibuka bora kinyume na ile inayofadhiliwa na serikali.

Ripoti hiyo inaitaja miradi inayofadhiliwa na wahisani kuwa miongoni mwa ile inayofanya vizuri zaidi nchini.Kwenye tathmini iliyoendeshwa katika Mwaka wa Kifedha wa Serikali wa 2019/20, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bi Nancy Gathungu, alisema hakukuwa na matatizo ya kifedha katika miradi hiyo.

Katika Wizara ya Afya, wakaguzi wa matumizi ya fedha walibaini tofauti kubwa za kifedha kwenye stakabadhi zilizowasilishwa kwao na idara mbalimbali.

Wataalamu wa masuala ya kiuchumi nchini wanasema kuwa hali hiyo inaonyesha mianya na mapungufu yaliyopo serikalini, ambako fedha zilizotengwa huporwa ama hutumiwa vibaya kutokana na ukosefu wa taratibu zifaazo katika kufuatilia matumizi yake.

“Kanuni kali ambazo huwepo katika usimamizi wa miradi inayoendeshwa na wafadhili huwanyima nafasi maafisa fisadi kupora fedha hizo.

“Sababu kuu ni kuwa wanajua wataitwa kueleza walivyozitumia. “Hata hivyo, hali ni kinyume kwa miradi ya serikali, ambapo kuna mianya mingi ambayo hutumiwa na maafisa waporaji kufuja fedha za umma,” akasema Bw Noah Wamalwa kutoka Taasisi ya Masuala ya Kiuchumi (IEA).

Hali imekuwa kama hivyo katika miaka ya awali, ambapo miradi iliyofadhiliwa na wahisani huwa inafanya vizuri katika ubora wake na matumizi ya fedha.

Kwenye ripoti ya kukagua matumizi ya fedha za serikali ya 2018/19, zaidi ya nusu ya miradi 188 inayoendeshwa na wahisani iliorodheshwa kusimamiwa kwa njia nzuri.

Miradi hiyo ilipata alama za juu sana kuhusu usimamizi wake.Kati ya miradi 10 bora nchini, saba imekuwa ile inayoendeshwa na wafadhili.

“Ripoti hizo ni muhimu sana ili kuhakikisha tunaendelea kupata ufadhili kutoka kwa wahisani. Hilo ndilo suala kuu ambalo wafadhili wengi wamekuwa wakizingatia,” ikasema taasisi hiyo.

You can share this post!

Masaibu yalivyomwandama Jaji Muchelule kwa miaka 14

DINI: Unayojiambia yatakuinua au kukufifisha, tafakari...