Makala

Mabilioni ya taabu katika familia za mabwanyenye wa Murang'a

May 17th, 2019 4 min read

Na MWANGI MUIRURI

KUMEJAA kilio katika familia za mabwanyenye mabilionea wa Murang’a ambao wameaga dunia hivi majuzi, wake zao na watoto wakilumbana hadi mahakamani kung’ang’ania mali.

Katika baadhi ya visa hivi, hata waliokuwa wapenzi wa pembeni wamejitokeza kung’ang’ania mali.

Wataalamu hushauri kuwa ni vyema kuwe na wosia wa ugavi wa mali, lakini hawa warithi wa mabilionea wankaonekana wazi kuwa hawatambui ushauri huo na pale ambapo wosia imeachwa, huo ndio kwanza wanapinga mahakamani wakitaka utupiliwe mbali na wao wawe ndio wa kujiamulia jinsi ya kugawana mabilioni hayo.

Miongoni mwa familia ambazo kwa sasa zinalumbana mahakamani ziking’ang’ania mabilioni ya wazazi wao ni pamoja na ile ya aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani John Michuki, mwanzilishi wa mapambano ya demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa Kenneth Njindo Matiba na pia ile ya mwanzilishi wa Benki ya Equity, John Mwangi Kagema.

Famlilia ya bwanyenye Gerishon Kirima ilikuwa imelumbana awali mahakamani kiasi kwamba kuna baadhi ya watoto wake ambao walikuwa
‘wamemnyakua’ ili aage dunia wakiwa ndio wameachiwa wosia wa ugavi wa mali. Ni kesi ambayo ilikuwa na hisia kali kiasi kwamba wana walikuwa
wakiwakana mama zao hadharani na kuwatusi mbele ya kamera za vyombo vya habari, huku utajiri wa baba yao wakati aliaga dunia ukibakia wa
kunyakuliwa hata na baadhi ya wanasiasa ambao walikuwa wamejipenyeza katika mirengo ya kulumbana ndani ya familia hiyo.

Oktoba 2013 ndipo mahakama iliwawezesha kuelewana na mzozo huo ukafika kikomo, familia hiyo ikiwa imepoteza takriban Sh20 bilioni katika
ukwasi uliokadiriwa kuwa unafikia kiasi cha Sh102 bilioni.

Mzozo huo wa Mzee Kirima na mabilioni yake ulikuwa sawa na ule wa bwanyenye mwingine wa Kaunti ya Murang’a kwa jina Samuel Kanogo Ritho
ambapo kabla ya kufariki alikuwa ameandika wosia uliotambua mkewe kuwa mratibu wa mali yake.

Mke huyo naye aliishia kufariki katika hali tata ambayo maafisa wa uchunguzi walisema alikuwa ametiliwa sumu katika chakula chake.

Marehemu Ritho ambaye alikuwa wakili aliaga dunia akiwa na ukwasi wa takriban Sh3.2 bilioni, utajiri ambao uliwafanya watoto wake wanne
kumgeuka mama yao ambaye hadi kifo cha baba yao, walikuwa wameoana kwa miaka 47.

Hatimaye mama huyo akifahamika kama Gladys Ritho aliaga dunia katika hospitali ya Mater jijini Nairobi akiwa na dalili za kula sumu
iliyoshukiwa ilikuwa imetiwa katika chakula.

Kwa sasa, kitinda mimba wa marehemu Michuki kwa jina Yvonne Wanja amewasilisha kesi mahakamani akitaka iamuliwe akabidhiwe ‘fungu lake’ la utajiri wa babake. Utajiri huo inakisiwa unafikia kiasi cha Sh65 bilioni na ambapo Bi Wanja anataka ugawanywe mara sita na apate kipande chake.

Katika familia ya Matiba, mjane Edith Matiba akiwa pamoja na wanawe wawili – Susan Wanjiku na Raymond Matiba – ameelekea mahakamani akitaka idhini ya kudhibiti mali ya Sh732 milioni.

Katika kesi hiyo, Bi Matiba pamoja na wawili hao kati ya watoto wake wote watano anasema kuwa “sisi watatu tumepata idhini ya wale wengine
wawili kuwa tuwe ndio wasimamizi wa mali hii.”

Katika familia ya bwanyenye mwingine wa Murang’a akifahamika kama Stephen Kirubi, bado ni hali ya vuta nikuvute wanawe wakilumbana mahakamani hadi sasa, miaka 13 baada ya baba yao kuaga dunia.

Mzozo wao unahusu shamba la hekari 150 ambalo liko katika Kaunti ndogo ya Maragua likidadisiwa kuwa lenye thamani ya Sh2 bilioni.

Na mwezi mmoja haukuisha baada ya John Mwangi Kagema kuaga dunia na kuacha ukwasi si haba ukiwa katika sekta za benki ya Equity ambayo
alikuwa mwanzilishi na pia ile ya Kilimo na ujenzi wa nyumba na makazi.

Hadi sasa, kumejitokeza wanawake watatu ambao wote wakidai  kuwa walikuwa mabibi zake huku nao baadhi ya watoto wake wakilumbana kuhusu
njia sawa ya kugawana ukwasi huo wake.

Tayari, Rais Uhuru Kenyatta ametaja mtindo huo unaoshika kasi kama usiofaa, uliojaa aibu ya kuangazia familia hizo kama zilizojaliwa ubinafsi na ulafi, akiwataka warithi kuzingatia majadiliano ya kifamilia ili kujiepusha na na kesi hizo.

Kaunti ya Murang’a imeorodheshwa kama iliyokuwa kielelezo bora cha jinsi ya kutekeleza uwekezaji katika miaka ya kuanzia 1930 na ambapo taifa likijipa uhuru wake mwaka 1963, eneo hilo lilikuwa limeweka msingi thabiti wa kuwa na mabilionea ambao walikuwa wakidhibiti asilimia 40 ya soko la hisa katika mwaka wa 2000.

Ngome ya wawekezaji

Katika mazishi ya bwanyenye Thayu Kabugi ambaye alikuwa mmiliki wa kampuni ya mafuta ya Astrol, Rais alisema Murang’a bado ni ngome
ya wawekezaji tajika ambao ni nguzo muhimu ya uchumi wa kitaifa.

Aliyekuwa Katibu maalumu katika Wizara ya Mawasiliano, Dkt Bitange Ndemo mwaka wa 2014 aliandika nakala ya utafiti aliyoipa anwani ‘The Mystery of Success‘ na ambapo alisema Murang’a itabakia kuwa msingi wa uwekezaji asili hapa nchini kwa miaka mingi ijayo.

Lakini mabilioni hayo ambayo yamekuwa yakirejelewa katika uwekezaji nchini sasa yanaonekana wazi kuwa yanakaribia kutawanyika kwa kuwa
kumeonekana kuwa wawekezaji hao ama walijisahau kimalezi na wakakosa kulea warithi wa kuwajibika au watoto hao kwa msukumo wa umero hawana maana ya mabilioni hayo.

“Ni kama kuna kasumba miongoni mwa watoto wa matajiri hapa Murang’a kuwa utajiri haufai kupaliliwa ili uendelee kudumishwa bali unafaa
kumegwa mara moja uishe. Kuna shida kubwa miongoni mwa watoto hawa wa matajiri kwa kuwa wana haraka ya kurithi mali bali sio waizalishe
ili ipokezwe vizazi; lakini ni iwarembeshee maisha kwa muda wa sasa wa uhai wao,” akateta aliyekuwa Kamishna wa Murang’a mwaka wa 2018, John Elung’ata.

Elung’ata aliteta kuwa alikuwa akipokea malalamishi mengi kutoka kwa wazazi wengi ambao walikuwa wakipokezwa vitisho na watoto wao kuwa ni lazima wagawe mali kwao huku wengine wakiwatolea vitisho vya mauti wazazi hao.

“Nia ya watoto hawa kuhangaisha wazazi kwa kiwango hicho ni kwa msingi tu wa kusukumania mali ili waipate kuidhibiti na waponde raha badala ya kuendeleza uratibu wa kudumisha uthabiti wa ukwasi huo,” akasema.