Michezo

Mabingwa Liverpool wapokezwa kichapo cha 4-0 uwanjani Etihad

July 3rd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MBWEMBWE za Liverpool baada ya kujinyakulia ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu zilipigwa breki na ladha ya sherehe za ufanisi huo kuyeyushwa na Manchester City waliowaponda 4-0 mnamo Julai 2, 2020, uwanjani Etihad.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool walikomesha subira ya miaka 30 ya kutia kapuni ufalme wa EPL mnamo Juni 25, 2020 baada ya Chelsea kuwacharaza Man-City 2-1 uwanjani Stamford Bridge.

Baada ya kuandaliwa gwaride la heshima na wenyeji wao uwanjani Etihad, Liverpool walianza kipindi cha kwanza ya mechi dhidi ya Man-City kwa matao ya juu huku kombora la Mohamed Salah katika dakika ya tano likigongwa mhimili wa lango la kipa Ederson Moraes.

Hata hivyo, Liverpool walionekana kuzidiwa maarifa katika kila idara kufikia robo ya kwanza ya kipindi cha pili na kusuasua kwao kukashuhudia Man-City wakipachika wavuni mabao matatu chini ya dakika 20.

Kiungo Kevin de Bruyne aliwafungulia Man-City ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa penalti kunako dakika ya 25 baada ya beki Joe Gomez kumchezea visivyo mshambuliaji Raheem Sterling ndani ya kijisanduku.

Sterling alipachika wavuni bao la pili katika dakika ya 35 kabla ya kiungo chipukizi Phil Foden kushirikiana vilivyo na De Bruyne na kuyafanya mambo kuwa 3-0 mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Man-City walipata bao lao la nne katika dakika ya 66 baada ya Alex Oxlade-Chamberlain aliyeingia uwanjani mwanzoni mwa kipindi cha pili kujaza nafasi ya Gomez kujifunga baada ya kuzidiwa na presha kutoka kwa Sterling.

Juhudi za Klopp kuwaleta uwanjani Naby Keita, Divock Origi, Neco Williams na Takumi Minamino kujaza nafasi za Georginio Wijnaldum, Roberto Firmino, Trent-Alexander Arnold na Sadio Mane mtawalia, ziliambulia pakavu.

Man-City wametawazwa mabingwa wa soka ya Uingereza katika kipindi cha misimu miwili iliyopita na pengo la alama moja pekee lilitamalaki kati yao ya Liverpool katika msimu uliopita wa 2018-19.

Huu ni msimu wa tatu pekee kati ya 11 iliyopita ambapo kocha Pep Guardiola ambaye ni mzawa wa Uhispania amekamilisha msimu bila ya kunyanyua taji la Ligi Kuu akiwa pia mkufunzi wa Man-City, Barcelona na Bayern Munich.

Ingawa pambano kati ya Man-City na Liverpool lilitarajiwa kuwa gumu zaidi kwa kila upande, liliishia kuwa mteremko mkubwa kwa masogora wa Guardiola ambao kwa sasa wanatazamiwa kupata hamasa zaidi ya kutia kapuni jumla ya mataji matatu msimu huu.

Baada ya kuhifadhi ubingwa wa League Cup, Man-City wanapigiwa upatu wa kutwaa Kombe la FA na kunyanyua ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Wamepangiwa kuvaana na Arsenal katika nusu-fainali ya Kombe la FA mnamo Julai 18 uwanjani Wembley, Uingereza kabla ya kupepetana na Real Madrid katika mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora ya UEFA. Walisajili ushindi wa 2-1 katika mkondo wa kwanza uwanjani Santiago Bernabeu, Uhispania mnamo Februari 26, 2020.

Riyad Mahrez aliyetokea benchi katika dakika ya 58 kujaza nafasi ya Gabriel Jesus alifunga bao mwishoni mwa kipindi cha pili ila likafutiliwa mbali na refa baada ya kurejelewa kwa video ya VAR iliyobainisha kwamba alikuwa amenawa mpira kabla ya kuujaza kimiani.

Ingawa walipachika wavuni mabao manne dhidi ya mabingwa wapya wa EPL, Man-City wamekuwa na matatizo makubwa katika safu yao ya ulinzi huku wakifungwa jumla ya mabao 33 kutokana na mechi 32 zilizopita.