Michezo

Mabingwa wa Chapa Dimba jijini ni wikendi

February 21st, 2020 2 min read

JEFF KINYANJUI na JOHN ASHIHUNDU

MABINGWA wa Chapa Dimba eneo la Nairobi watajulikana wikendi hii, timu nane zikipepetana katika shule ya Jamhuri High School jijini Nairobi.

Katika kitengo cha wavulana, watetezi South B United kutoka tarafa la Starehe walishindwa kutinga hatua ya makundi, na sasa bingwa mpya atajulikana Jumapili.

Lakini Acakoro kutoka mtaa wa Korogocho wanarejea tena kutetea ubingwa wa taji la wasichana watakapokabiliana na St Anne Eaglets kesho Jumamosi katika nusu-fainali.

Akizungmza kuhusu mechi ya kesho, kocha Awuor alieleza matumaini makubwa ya kikosi chake kushinda na kuhifadhi ubingwa.

“Tumejipima nguvu na Ulinzi Starlets Jumatano katika mechi ya kirafiki na tukashinda 3-0, hivyo nina matumaini makubwa ya vijana wangu kuandikisha matokeo ya kuridhisha dhidi ya St Anne,” alisema.

“Kama mabingwa watetezi, kila mtu atakuwa akitulenga, lakini tumejipanga vilivyo kwa upinzani wowote ule,” aliongeza. Lakini mwenzake Stephen Babu wa St Anne alimuonya asitarajiea mtermko.

“Sina mchezaji anayeuguza jeraha, na kila mtu yuko tayari kucheza. Tunalenga ubingwa, na tuna kila sababu ya kuutwaa,” alisema.

Katika kitengo cha wavulana, Hakati Sportiff watakutana na Brookshine Academy katika nusu-fainali huku kocha wao, Charles Nyongesa akisisitiza kuwa lengo lao ni kushinda taji.

“Hatuwaelewi wapinzani wetu vyema, lakini tumejiandaa vizuri kwa muda wa miezi miwili. Tutacheza mchezo wetu tukilenga ushindi na kufuzu kwa fainali,” aliongeza.

Timu zitakazoibuka na ubingwa katika vitengo vyote viwili zitaondoka na Sh200,000, kila mmoja, huku zitakazomaliza katika nafasi ya pili zikipokea Sh100,000, huku wachezaji watakaong’ara wakitunukiwa tuzo mbali mbali.

Washindi wa taji la kitaifa watapokea Sh1 milioni, na baadaye timu ya mzeto itaundwa kwa ajili ya kuzuru nchini Uhispania kwa kambi ya siku 10 ambapo watacheza mechi za kujipima na wanasoka kutoka vituo vya klabu maarufu za LaLiga.

Tayari timu za Tumaini School kutoka Makueni na Isiolo Starlets zimefuzu kuwakilisha Kanda ya Mashariki, zikiungana na Berlin FC ya Garissa ya wavulana ikiwakilisha Kanda ya Kaskazini Mashariki.

Kanda ya Pwani itawakilishwa na Yanga FC ya Malindi na Kwale Ladies huku Kanda ya Kati ikiwakilishwa na Falling Waters ya Laikipia na Ulinzi Youth ya Nanyuki.

Ratiba:

Nusu-fainali Jumamosi, wavulana: Brookshine Academy na Hakati Sportiff – saa tano asubuhi, KSG na Dagoretti High School (saa tisa).

Wasichana: Kibagare Girls School na Beijing Raiders (saa tatu asubuhi), Acakoro Ladies na St Annes Eaglets (saa saba).