Michezo

Mabingwa wanne wa dunia ni miongoni mwa wakali watakaonogesha Kip Keino Classic

September 23rd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

EDRIS Muktar ni miongoni mwa mabingwa wanne wa dunia ambao wamethibitisha kunogesha riadha za kimataifa za Kip Keino Classic uwanjani Nyayo, Nairobi mnamo Oktoba 3, 2020.

Mabingwa wa dunia raia wa humu nchini ambao watashiriki pia kivumbi hicho ni Timothy Cheruiyot (mita 1,500), Conseslus Kipruto (mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji) na Hellen Obiri (mita 5,000).

Muktar ambaye alihifadhi ufalme wa mbio za mita 5,000 katika Riadha za Dunia za 2019 jijini Doha, Qatar ataongoza Waethiopia wenzake katika mbio hizo za mizunguko 12 jijini Nairobi.

Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) limethibitisha kwamba mbio za Kip Keino Classic zimevutia wanariadha 120 kutoka mataifa 30 tofauti kufikia sasa.

Hata hivyo, mkurugenzi wa mbio hizo, Barnaba Korir, amesema kwamba wanariadha wa haiba kubwa zaidi kutoka humu nchini wanatazamiwa kuthibitisha kushiriki kwao kufikia Septemba 25 ambayo ni siku ya makataa.

Naibu Rais wa AK, Paul Mutwii amefichua kwamba majaribio katika fani za mita 200, mita 400 na mita 800 yatafanywa mnamo Septemba 26 ili kufanyia majaribio vifaa mbalimbali katika uwanja wa Nyayo ambao umekuwa ukikarabatiwa kwa miaka mitatu iliyopita.

Kati ya watimkaji wanaotazamiwa pia kunogesha mbio za Kip Keino Classic mabingwa wa zamani wa dunia na washindi wa nishani za fedha katika Riadha za Dunia za 2019, mabingwa wa mbio za dunia za nyika, washindi wa Olimpiki na miamba wa Jumuiya ya Madola.

Fani zitakazoshindaniwa katika kivumbi hicho ni kuruka mara tatu, urushaji wa kisahani, mbio za mita 200, mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji kwa upande wa wanawake na wanaume.

Vitengo vingine ni urushaji mkuki (wanaume), mbio za mita 400, mita 800m, mita 1,500 na mita 5,000 kwa upande wa wanawake na wanaume.

Mbali na Muktar, 26, Waethiopia wengine watakaonogesha mbio za mita 5,000 ni mshindi wa nishani ya fedha duniani Selemon Barega na Hagos Gebrhiwet aliyeridhika na nishani ya fedha katika Olimpiki za Rio 2016. Hagos alitwaa pia nishani ya shaba katika Riadha za Dunia za 2015 jijini Beijing, China na akaridhika na fedha katika Riadha za Dunia za 2013 jijini Moscow, Urusi.

Mbio hizo zimevutia pia Waethiopia Haile Talahun na Berihu Aregawi watakaotoana jasho na Wakenya Jacob Krop, Nicholas Kimeli, Rhonex Kipruto na Waganda Samuel Kibet na Oscar Chelimo.

Francine Niyonsaba ambaye ni bingwa wa mita 800 nchini Burundi atashiriki kivumbi cha mita 5,000 kitakachomjumuisha Obiri na wanariadha wengine wa haiba kutoka Kenya na Ethiopia wakiemo

Margaret Chelimo, Beatrice Chebet, Agnes Tirop na Abersh Minsewo.

Kipruto atafufua uhasama wake na mshindi wa medali ya shaba dunia katika mita 3,000 kuruka viunzi na maji, Soufiane El Bakkali wa Morocco.

Bingwa wa zamani wa kitaifa katika mbio za mita 100 na mita 200, Mike Mokamba na Steve Mwai watanogesha kitengo cha mita 200 ambacho pia kina Arthur Cisse wa Ivory Coast. Cisse aliibuka wa pili katika mbio za mita 100 (sekunde 10.04) kwenye duru ya Diamond League iliyoandaliwa jijini Roma, Italia mnamo Septemba 17, 2020.

Eunice Kadogo ndiye Mkenya wa pkee katika mbio za mita 200 kwa upande wa wanawake. Bingwa wa kitaifa katika mbio za mita 400 Alphas Kishoyian atashirikiana na Collins Omae huku Hellen Syombua, Joan Cherono Mary Moraa wakinogesha mbio hizo kwa upande wa wanawake.