Michezo

Mabingwa watetezi Bayern Munich wafuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA bila kushindwa kundini

December 10th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Bayern Munich, walikamilisha kampeni zao za makundi msimu huu wa 2020-21 kwa kusajili ushindi wa 2-0 dhidi ya Lokomotiv Moscow mnamo Disemba 9, 2020 uwanjani Allianz Arena, Ujerumani.

Ushindi huo wa Bayern uliwawezesha kufikisha rekodi ya kutoshindwa katika jumla ya mechi 17 mfululizo za UEFA.

Mnamo 2019-20, miamba hao wa Ujerumani wanaonolewa na kocha Hansi Flick, walishinda mechi zao zote 11 katika kampeni za UEFA na hatimaye kunyanyua taji baada ya kucharaza Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa 1-0 kwenye fainali iliyoandaliwa jijini Lisbon, Ureno.

Kufikia sasa, Bayern wameambulia sare mara moja pekee kwenye UEFA ambapo walitoshana nguvu kwa matokeo ya 1-1 dhidi ya Atletico Madrid ya Uhispania mnamo Disemba 1, 2020 uwanjani Wanda Metropolitano.

Wakicheza dhidi ya Lokomotiv mnamo Disemba 9, Bayern walifungiwa na Niklas Sule na Eric Maxim Choupo-Moting katika dakika za 63 na 80 mtawalia.

Atletico walisonga mbele kwa hatua ya 16-bora katika Kundi A baada ya kupiga Red Bull Salzburg 2-0 nchini Austria. Ushindi huo wa Atletico wanaotiwa makali na kocha Diego Simeone, unamaanisha kwamba Salzburg kwa sasa wanashuka hadi Europa League baada ya kumaliza kampeni za makundi katika nafasi ya tatu kwa alama nne, moja mbele ya Lokomotiv waliovuta mkia.

Bayern walikosa huduma za mshambuliaji wao matata Robert Lewandowski katika mechi iliyowakutanisha na Lokomotiv mnamo Disemba 9. Nahodha huyo raia wa Poland anauguza jeraha la misuli ya miguu.

Bayern wangalifunga mabao mengi katika kipindi cha pili ila kipa Guilherme Costa Marques wa Lokomotiv akafanya kazi ya ziada na kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na Serge Gnabry, Sule, Jamaal Musiala na Leroy Sane aliyeagana na Manchester City mwishoni mwa msimu wa 2019-20.

Jaribio la pekee ambalo Lokomotiv walipata langoni mwa Bayern ni kombora ambalo kipa Manuel Neuer alivurumishiwa na Maciej Rybus mwishoni mwa kipindi kwa kwanza.