Mabingwa watetezi Man-City wakomoa Wycombe na kutinga hatua ya 16-bora katika Carabao Cup

Mabingwa watetezi Man-City wakomoa Wycombe na kutinga hatua ya 16-bora katika Carabao Cup

Na MASHIRIKA

RIYAD Mahrez alifunga mabao mawili na kusaidia waajiri wake Manchester City ambao ni mabingwa watetezi wa Carabao Cup kutinga hatua ya 16-bora ya kipute hicho kwa kuponda Wycombe Wanderers 6-1 mnamo Jumanne usiku.

Wageni Wycombe walijiweka kifua mbele katika dakika ya 22 kupitia Brandon Hanlan kabla ya kiungo Kevin de Bruyne kusawazisha mambo dakika saba baadaye.

Kusawazisha huku kuliwapa Man-City motisha zaidi ya kuvamia lango la wageni wao na wakafunga mabao mengine kupitia Mahrez, Phil Foden na Ferran Torres kabla ya chipukizi Cole Palmer, 19, kutokea benchi na kupachika wavuni goli la sita baada ya kumzidi ujanja kipa David Stockdale.

Mechi ilitoa nafasi kwa kocha Pep Guardiola kuwapa chipukizi Conrad Egan-Riley, Luke Mbete, Finley Burns, Josh Wilson-Esbrand na Romeo Lavia fursa ya kudhihirisha uwezo wao kutandaza boli uwanjani.

Kati ya wote hao, ni beki Wilson-Esbrand ndiye aliyeridhisha zaidi huku akichangia bao la pili lililofumwa wavuni na Mahrez ambaye ni raia wa Algeria.

Ushindi wa Man-City uliendeleza rekodi nzuri ya kutoshindwa kwa Man-City katika Carabao Cup tangu Oktoba 2016. Miamba hao wa soka ya Uingereza sasa wametinga hatua ya 16-bora ya Carabao Cup kwa mara ya tano mfululizo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Serikali yatangaza vita na watengenezaji pombe haramu Mlima...

DP yamteua Spika Muturi kuwa mgombeaji urais