Michezo

Mabingwa watetezi UEFA wasalimu amri

March 7th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MADRID, Uhispania

MATUMAINI ya Real Madrid kusonga mbele na kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya nne mfululizo yaliangamia baada ya kufungwa 4-1 na Amsterdam Ajax ya Uholanzi na kubanduliwa nje mechi ya kutafuta nafasi ya kufuzu kwa robo-fainali.

Vijana hao wa kocha Santiago Solari waliingia uwanjani mwao Santiago Bernabeu wakijivunia ushindi wa 2-1, huku wakihitaji sare ya aina yoyote na kusonga mbele.

Kichapo cha 4-1 kilikuwa cha kwanza kikubwa kwa Madrid ugani mwao Bernabeu tangu chapwe 3-0 na CSKA Moscow mwezi Desemba.

Kushindwa kwao kadhalika kumekuja siku sita baada ya kubanduliwa nje ya michuano ya Copa del Rey na Barcelona, huku wakiwa na mwana wa pointi 12 nyuma ya wapinzani hao wao wa La Liga.

Kwa mara ya kwanza mfululizo tangu 2015 ambao ni muda wa miezi 42, Real Madrid wamebanduliwa nje ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.

Waliwekewa matumaini makubwa baada ya kutwaa taji hilo mara tatu mfululizo tangu msimu wa 2015-16.

Real Madrid wametinga hatua ya nusu-fainali ya michuano hiyo kila msimu tangu wabanduliwe nje katika hatua ya 16 bora na Lyon ya Ufaransa mnamo 2010, ambao ulikuwa mwaka wa kwanza Cristiano Ronaldo kuwachezea.

Mwaka 2019 mfungaji wao bora Karim Benzema alifanikiwa kufunga mabao manne pekee katika michuano hiyo, nyuma ya Robert Lewandowski (manane), Lionel Messi wa Barcelona (sita) au Dusan Tadic (pia sita).

Kadi nyekundu

Nahodha wao, Sergio Ramos ambaye aliikosa mechi hiyo kutokana na kadi nyekundu aliyopewa katika mkondo wa kwanza aliitazama mechi hiyo akiketi na mashabiki waliofika uwanjani.

Baada ya kichapo hicho, mashabiki wa Madrid waliondoka uwanjani kimya kimya bila kulalamika, huku wengine wakidhania huenda kuchelewa kwa klabu hiyo kusajili staa wa kujaza nafasi ya Ronaldo kumechangia matokeo mabaya katika mechi zao muhimu.

Gareth Bale aliyedhaniwa kujaza nafasi hiyo, hakuanza baada ya kucheza vibaya mwishoni mwa wiki.

Lakini, hata baada ya kuingia baada ya Lucas Vazquez kuumia, raia huyo wa Wales hakusaidia pakubwa kuokoa jahazi.

Aliyekuwa kocha wa Manchester United na Real Sociedad, David Moyes alisema, baada ya Ronaldo kuondoka, Madrid ilitarajiwa kuwategemea Luka Modric, Toni Kroos na Sergio Ramos, lakini huenda wakaondoka hivi karibuni kutokana na umri wao mkubwa.

Toni Kroos wa Real Madrid aondoka uwanjani Machi 5, 2019, ambapo Real Madrid CF ilipigwa na Ajax mabao 4-1 uwanjani Santiago Bernabeu. Picha/ AFP

Alisema ni jukumu la wakuu wa klabu hiyo kuanza kutafuta mapema wachezaji wa kujaza nafasi za nyota hao.

“Bila Ronaldo, wameshindwa kufunga mabao ya kutosha, mbali na kubanduliwa nje mbele ya mashabiki wao wengi waliomiminika katika uwanjani,” aliongeza.

Katika michuano hii msimu huu, Real Madrid ambao ni mabingwa mara 13, walishinda mechi nne. Ugani Bernabeu, Ajax ilipata mabao kupitia kwa Dusan Tadic (2), Hakim Ziyech na Lasse Schone. marco Asensio waliwafungia wenyeji bao la kufutia machozi, zikibakia dakika 20 mechi kumalizika.