Michezo

Chipukizi wa Kibera Saints sasa watawala ligini

November 18th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

KIKOSI cha Kibera Saints kilichupa juu ya jedwali ya kampeni za kufukuzia taji la Nairobi West Regional League (NWRL) kiliponyoa Kemri FC mabao 2-0 kwenye mchezo uliyopigwa uwanjani Woodley Kibera, Nairobi.

Nao chipukizi wa timu ya KYSA Karengata na Kibera Lexus zilivuna alama tatu muhimu baada ya kila moja kubeba mabao 2-0 dhidi ya Kenya Forest Service (KFS) na Silver Bullets mtawalia.

Wachezaji wa Kibera Saints ambao hunolewa na kocha, William Mulatya iliingia mjegoni ikilenga kufanya kweli baada ya kutoka sare bao 1-1 na Mafande wa Nairobi Prisons wiki iliyopita.

Wapigagozi hao walionyesha mechi safi na kuwazidi wapinzani wao maarifa. Mchezaji mwepesi, Felix Onyango alibahatika kuibuka shujaa alipofunga mara mbili na kubeba kikosi hicho kutwaa usukani wa ngarambe hiyo.

”Bila shaka tunashukuru sana kwa ushindi huo ambapo ni dhahiri shahiri tunapiga hatua ingawa tunafahamu kibarua kizito mbele yetu kwenye mechi sijazo,” kocha huyo alisema na kuwataka wachezaji wake kamwe kutolaza damu.

Nayo KYSA Karengata iliandikisha ufanisi huo kutokana na mabao ya Stephen ‘Brayo’ Odhiambo na Victor Oketch. Nao Billy Onyango na Bernard Onyango wa Kibera Lexus kila mmoja aliitingia bao moja.

Nayo KSG Ogopa FC inayoshiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza muhula huu ilikomoa Riruta United (Makarios 111 FC) na kurukia mbili bora kwa kukusanya alama kumi, moja mbele ya WYSA United haikucheza wikendi.