Mabinti wabwaga wavulana

Mabinti wabwaga wavulana

Na BENSON MATHEKA

MATOKEO ya mtihani wa kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) wa 2020 yaliyotolewa jana, yalikuwa na maajabu ya aina yake katika historia ya mtihani huo nchini.

Kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka mingi, shule za msingi za umma zimefanya vyema kuliko za kibinafsi kwa kutoa wanafunzi 10 miongoni mwa 15 bora kote nchini.

Shule hizo za umma pia ziliandikisha nafasi nne bora kitaifa, kinyume na miaka ya awali ambapo zile za kibinafsi zimekuwa zikiwika kwa kishindo.

Wasichana nao wamevunja rekodi kwa kuwabwaga wavulana walipotwaa nafasi za kwanza tatu, tofauti na miaka iliyotangulia ambapo wavulana na wasichana walikuwa wakikabana koo katika nafasi 10 bora.

Faith Mumo wa shule ya Kari Mwilu katika Kaunti ya Makueni, alikuwa mwanafunzi bora kitaifa kwa alama 433.

Tukio lingine la kihistoria ni kuwa kwamba ilikuwa mara ya kwanza KCPE kufanywa mwezi Machi na matokeo kutangazwa wiki mbili baada ya mtihani kukamilika, huu ukiwa muda mfupi zaidi matokeo ya mtihani kutolewa.

Mtihani huo ulifanyika chini ya masharti makali ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona baada ya kalenda ya elimu kuvurugwa na janga hilo mwaka jana.

Mtihani huo ulioahirishwa Novemba mwaka jana kwa sababu ya janga la corona ulianza Machi 22 na kukamilika Machi 24, 2021.

Ilikuwa mara ya kwanza mtihani wa kitaifa kuahirishwa kwa sababu ya janga la kimataifa, ambapo shule zilifungwa kwa miezi tisa mwaka jana. Watahiniwa walirudi shuleni Disemba mwaka jana kujiandaa kwa mtihani.

Jumla ya watahiniwa 1,179,192 walifanya mtihani huo katika vituo, wakiwa wameongezeka kutoka 1,083,456 waliofanya mtihani huo 2019.

Naomi Njoki aliyepata alama 403 kwa KCPE ashangiliwa kwa kuiletea faraja Shule ya Msingi Pink Roses, Githunguri, Kaunti ya Kiambu. Picha/ Hisani

Licha ya janga la corona kuvuruga kalenda ya elimu, wanafunzi waliandikisha matokeo mazuri na kufanya Waziri wa Elimu Profesa George Magoha kuwamiminia sifa tele.

“Kuna waliodhani kwamba matokeo ya mwaka huu yangekuwa mabaya kwa sababu ya kuvurugika kwa kalenda ya elimu. Shetani ashindwe kwa kuwa wanafunzi wote watajiunga na shule za sekondari,” alisema waziri.

Tofauti na miaka ya awali ambapo wanafunzi waliopatikana wakihusika na udanganyifu walikuwa wakinyimwa matokeo, mwaka huu watakabidhiwa matokeo.

Licha ya matokeo kutolewa jana, wanafunzi watakaa nyumbani hadi Julai watakapojiunga na kidato cha kwanza.

Awali matokeo yalikuwa yakitolewa mwishoni mwa Novemba au Disemba na wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza Januari.

Pia kwa mara ya kwanza katika historia ya mtihani huo, kaunti za maeneo ya mashambani za Pokot Magharibi, Baringo, Bomet, Kericho na Bungoma zilisajili idadi kubwa ya watahiniwa wa umri mdogo wa chini ya miaka 12. Awali, ni shule za maeneo ya mijini zilizosajili watahiniwa wa umri mdogo.

Idadi ya wanafunzi walio na umri mdogo pia iliongezeka kutoka 20,086 mwaka wa 2019 hadi 26,378 mwaka jana.

Kutolewa kwa matokeo mapema kumekuwa mbinu ya kuzuia udanganyifu katika mitihani, ambapo baadhi ya shule hasa za kibinafsi zilidaiwa kuwahonga maafisa wa Knec ili ziweze kupatiwa alama bora.

Kutolewa kwa matokeo mapema pia kumesaidia wazazi kujua mapema shule za sekondari ambazo watoto wao wanachaguliwa kujiunga nazo ili waweze kujiandaa.

Wazazi na watahiniwa waliweza kujua matokeo yao mara baada ya Prof Magoha kuyatangaza kupitia ujumbe mfupi wa simu.

You can share this post!

Wakulima wa Mataara wapinga uchaguzi wa ghafla

Matokeo ya somo la Kiswahili yaimarika pakubwa