Michezo

Mabinti waomba wapigwe jeki kisoka

June 15th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE 

TIMU za kina dada za ngarambe ya Ligi Kuu (KWPL) zimeibua mazito yanayogonga wakuu wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF). Kiukweli kwa sasa hali si hali kabisa. Kisa? Hali ni ngumu zaidi.

Dah! Dunia inapitia wakati mgumu lakini hapa Kenya hali ni kama shamba la mawe. Sio virusi hatari vya corona, sio mvua, sio mafuriko, sio njaa! Hakika hakieleweki.

Hayo tisa. Kumi vikosi vya soka la wanawake vinamtaka rais wa FKF, Nick Mwendwa asiviweke katika kaburi la sahau katika mpango wa chombo hicho na serikali wa kuwapiga jeki wanasoka. Ukweli wa mambo ni kwamba pia wanasoka wa kike wamejikuta kwenye wakati mzito kutokana na janga la corona.

”Wanawake ni wanawake, ninaamini muda huu ni hatari na rahisi kupoteza wanasoka wa kike, amesema kocha wa Ulinzi Starlets, Joseph Wambua Mwanzia inayoshiriki Ligi Kuu. Kocha huyo ametamka hayo baada ya kampuni ya mchezo wa kubas hiri ya Betika kutoa msaada kwa klabu za Ligi Kuu (KPL) na Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL).

Katika mpango mzima wachana nyavu wa vipute hivyo wana sababu ya kutabasamu baada ya kupokea Sh5.3 milioni wakati huu wa mlipuko wa corona.

Timu ya Wadadia LG Mumias.

Kampuni hiyo ilitoa msaada huo wiki moja baada ya serikali kupitia wizara ya michezo kuhitisha majina ya wachezaji wa ligi tano za humu ili kuwapiga jeki. Msaada huo uliendea wapigagozi 587 washiriki wa klabu 17 za KPL na 19 za BNSL.

”Tunatoa mwito kwa FKF pia itafute namna itakavyowasaidia wachezaji wa kike maana mwanamke ni rahisi kusepa na kupigia chini shughuli za michezo,” akasema. Alisisitiza kuwa FKF ingehifadhi fedha hizo kwa muda ili kuzigawa baada ya kupokea misaada zaidi.

”Kipindi hiki viongozi wetu wanastahili kuwa makini zaidi ili kuokoa washiriki wa soka la wanawake kwa kuzingatia wanaweza kutokomea kwingine maana hamna wanalofanya,” alisema kocha wa Wadadia LG, Richard Sumba.

Wachezaji wa Trans Nzoia Falcons

Klabu za kinyangányiro hicho zimejiweka vizuri kushiriki michuano ya msimu huu itakapoanza tena baada ya corona kuisha. SEP Oyugis FC ya kocha, Morris Onyango inayoshiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza anaamini itafanya kweli.

Kocha huyo amesema ”Tunatarajia kujituma mithili ya mchwa kukabili wapinzani wetu kwenye mechi za msimu huu.” Klabu hiyo ilinasa wachana nyavu wawili wa kitaifa ili kuchochea wenzao kuwania taji hilo. SEP Oyugis inajivunia kusajili Pauline Musungu kutoka Vihiga Queens na Anita Adongo aliyekuwa akichezea Alliance FC ya Tanzania.

Kampeni za kipute hicho zitajumuisha vikosi kama Ulinzi Starlets, Vihiga Queens, Thika Queens, Makalonders, Wadadia LG, Kisumu Allstarlets,Trans Nzoia Falcons, Gaspo Women na SEP Oyugis kati ya zingine.

Mchezaji wa Thika Queens (jezi nyekundu) na mwenzake wa Makolanders FC kwenye mchezo wa awali.