Makala

Maboga yana manufaa mengi kiafya

March 14th, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

WENGI wanayajua kama ‘malenge’, lakini jina halisi kwa lugha ya Kiswahili ni ‘maboga’.

Miaka ya awali, yalihusishwa na uchochole kwa kuaminika kuliwa na wasiojiweza.

Hata hivyo, dhana hiyo sasa imepitwa na wakati na yanaliwa na yeyote yule, kwa ajili ya manufaa yake tele kiafya.

Mtaalamu James Murage akitoa mafunzo ya upanzi, utunzaji, mavuno na soko la maboga, katika maonyesho ya kilimo ya shamba la Mariira, Kigumo, kaunti ya Murang’a mnamo Machi 9, 2019. Picha/ Sammy Waweru

Faida kiafya

Maboga yamesheheni Protini na madini kadhaa kama vile Chuma, Kopa, Maginizia, Manganizi na Zinki. Mbegu zake zinasemekana kusaidia kuepushia mlaji zaidi ya magonjwa 10 kama; ugonjwa wa moyo, Saratani, Kisukari na uvimbe.

Aidha, mbegu za maboga zina mafuta ya Omega 3 ambayo ni miongoni mwa mafuta muhimu mwilini.

Hizo ni tija chache tu kuzitaja, zinazotokana na zao hili.

Maonyesho ya kilimo

Mnamo Machi 8 na 9, 2019, shamba la Mariira lililoko kaunti ndogo ya Kigumo, Murang’a liliandaa maonyesho ya kilimo yaliyoalika wanazaraa kutoka kona mbalimbali za nchi.

Ni katika hafla hiyo ambapo Taifa Leo Dijitali ilitangamana na wakulima na wataalamu wa kilimo mbalimbali.

Maboga ni baadhi ya mimea iliyovutia, na ni kupitia kampuni ya Safari Seeds ambapo wakulima wa zao hili walipata mwanya wa kipekee kuelimishwa kulihusu.

Katika mazungumzo, Daniel Mwangi, mkulima, aliibua mjadala akihoji ni maboma machache mno yanayopanda maboga, ikilinganishwa na miaka ya zamani; sababu ni gani?

Upungufu

Mkulima huyu alieleza kwamba bei ya zao hili imedorora, na huenda ndiyo sababu wakulima wameacha kuyapanda kwa wingi. “Ukitembea katika maboma mengi hasa eneo la Kati ni nadra kupata maboga kama ilivyokuwa miaka ya awali. Inaonekana watu hawajui manufaa yake kiafya,” alisema.

James Murage, mtaalamu wa kilimo Safari Seeds alifungua jamvi la somo lake kwa kuorodheshea Bw Mwangi manufaa ya maboga na mbegu zake kiafya.

“Madaktari hushauri wagonjwa kula maboga kwa wingi, hasa mbegu zake zilizosheheni madini aina ya Zinc. Watoto hulishwa kwa wingi kwa ajili ya manufaa yake. Ni muhimu kutaja kwamba mbegu zake pia zinasagwa na kuchanganywa na unga wa ngano kupika chapati,” akafafanua Bw Murage.

Kauli ya mdau huyu inaungwa mkono na Regina Kimani, mkulima wa maboga eneo la Kambiti, Murang’a.

Shabaha yake ilipania kujua mbinu bora kuongeza kiwango cha mazao.

Majani ya maboga huliwa kama mboga kwa uandamanisha na ugali, na pia kutumika katika mapishi ya ‘mukimo’; mchanganyiko wa kande, viazi mbatata, na mboga.

Bi Regina alimtaka Murage kuchanganua suala hilo, ingawa mtaalamu huyo alishauri wakulima kuepuka kuyachuma akihoji majani ndiyo kiini cha chakula cha maboga.

“Kitaalamu hairuhusiwi kuyachuma. Majani ndiyo chakula cha maboga. Miale ya jua ni muhimu kwa mimea na hulakiwa na majani,” alidokeza Bw Murage.

Upanzi

Mtaalamu huyu alisema upandaji wa zao hili ni rahisi mno, ukilinganishwa na mimea mingine. Kuna njia mbili za kuyapanda; kutumia miche au kupanda mbegu moja kwa moja shambani. “Miche ya maboga huchukua siku 21 kitaluni. Mbinu bora ni ile ya kupanda mbegu moja kwa moja,” akasema Murage.

Shamba linapaswa kulimwa jembe moja kuenda chini, na kuandaa mashimo yenye urefu wa nusu futi. Nafasi ya shimo moja hadi lingine kitaalamu inapendekezwa kuwa futi nne kwa nne, mraba. Bw Daniel Mwangi alihoji pembejeo hasa fatalaiza imekuwa ghali mno na ni mojawapo ya kizingiti kikuu katika shughuli za kilimo. Mkulima huyu aliomba kujua iwapo mboleahai, yaani ya mifugo inafanikisha ukuzaji wa maboga. “Iwapo sina pesa za kununua fatalaiza, inawezekana nitumie mbolea ya mifugo na nipate mazao bora?” Aliuliza, akifafanua ubora aliomaanisha ni kupata maboga mengi.

Mdau Murage alihimiza umuhimu wa kuzingatia kilimohai, utumizi wa mbolea ya mifugo ikiwa mojawapo. Alisema wakulima wasilenge kupata maboga mengi, ila maboga makubwa bora yatayopiku bei ya yale madogo. Ili kufanikisha hilo, upanzi wake uafikie vigezo vya kilimo kitaalamu.

“Wakulima watumie mbolea iliyoiva sawasawa (akimaanisha iliyooza, ichanganywe na mchanga. Mashimo yamwagiliwe maji kabla ya kupanda mbegu,” akaelekeza. Huchipuka kati ya siku 5 hadi 7.

Mazao na soko

Ili kupata maboga makubwa, mkulima anashauriwa kuondoa matawi (desuck) na maua yaliyozidi matano. “Shughuli hii ifanywe baada ya siku 45. Salia na maua matano, ambayo yatazalisha maboga makubwa bora,” anasema Murage. Anaeleza kwa kufanya hivyo maua yaliyochana hayatakuwa na mashindano ya lishe; maji na mbolea.

Sokoni, boga lenye uzito wa kilo 5-8 huuzwa kati ya Sh150 hadi Sh200.

Mtaalamu huyu anasema yanapita kilo 10 yana uwezekano wa kugharimu zaidi ya Sh400.

“Nimepokea oda nyingi sana kutoka hospitali mbalimbali eneo la Kati, wakulima ndio hawapo,” anasema.

Maboga aina ya Dora

Safari Seeds, kampuni ya tafiti za kilimo, imevumbua aina mpya ya maboga, Dora, yanayovunwa siku 90 yaani miezi mitatu, baada ya upanzi.

Maboga mengine huvunwa kati ya miezi mitano hadi sita baada ya kupanda.

Bw Murage anasema ekari moja inahitaji gramu 500 ya mbegu za Dora, yenye jumla ya mbegu 4,000.

Kipimo hiki kinagharimu Sh350.

Ni vigumu maboga kuathiriwa na wadudu au magonjwa ya mimea.

Hata hivyo, nzi wa matunda anapodunga boga kwa kufyonza maji yake, husababisha kuoza.

Hudhibitiwa kwa kupulizia dawa dhidi ya wadudu. Baada ya mavuno, maboga yana uwezo wa kuhifadhiwa kwa muda wa mwaka mmoja.