Habari Mseto

Mabunge mawili ya kitaifa sasa yalegeza masharti ya corona

September 17th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Kitaifa na lile la Seneti yamelegeza masharti ambayo yalikuwa yakitekeleza kwa ajili ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Hii ni kufuatia kupungua kwa idadi ya visa vya maambukizi vinavyonakiliwa kila siku tangu mwishoni mwa mwezi jana.

Katika mabadiliko yaliyotangazwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi Jumanne alasiri, idadi ya wabunge watakaoruhusiwa wakati mmoja katika ukumbu mkuu wa mijadala sasa imeongezwa hadi wabungr 112 kutoka wabunge 60. Idadi hii ni kando na Spika, karani na maafisa wane wasaidizi.

Tangu mwezi wa Aprili ni wabunge 60 pekee ndio wamekuwa wakiruhusiwa katika ukumbi huu wakati mmoja kama hatua  ya kuzuia msambao wa Covid-19.

“Baada ya ukaguzi uliofanywa na Wizara ya Afya, sasa ukumbi mkuu wa mijadala itasitiri wabunge 112 wakati mmoja badala ya 60 ilivyo wakati huu. Mabadiliko hayo yataanza kutekelezwa katika kikao Alhamsi Septemba 16, 2020,” Bw Muturi akawaambia wabunge  Jumanne alasiri.

Na idadi ya wabunge watakaoruhusiwa kutumia vyumba vya mikutano ya kamati za bunge katika Jumba la Continental, wakati mmoja, imeongezwa kutoka 10 hadi 15.

Katika ukumbi wa ibada kwa Wakristo jumla wabunge 15 wataruhusiwa kuutumia kwa wakati mmoja badala ya wabunge watano ilivyokuwa tangu Aprili huku vyumba vinavyotumiwa na Waislamu kusali vitabeba watu tisa kwa wakati mmoja badala ya wane.

Spika Muturi pia alisema mikahawa katika majengo ya bunge imefunguliwa na itatumiwa na wabunge pekee wala sio wageni.

“Wageni hawataruhusiwa ndani ya majengo ya bunge isipokuwa isipokuwa wale ambao wamealikwa kutoa ushahidi katika Kamati za Bunge,” akaeleza.

Kwa upande wao maseneta Jumanne walipitisha hoja ya kuwawezesha kufanya vikao viwili kwa wiki badala ya kikao kimoja kama ambavyo wamekuwa wakifanya tangu Aprili mwaka huu.

Akiwasilisha hoja hiyo, kiongozi wa wengi Samuel Poghisio alisema hatua hiyo imechukuliwa ili kuipa Seneti nafasi ya kukamilisha mrundiko wa shughuli muhimu ambazo zimesalia.

“Kwa kufanya kikao kimoja kila siku, bunge hili limejipata na mrundiko mkubwa wa kazi. Hii ndio maana uongozi umewasilisha hoja ya kuruhusu kufanyike vikao viwili kila wiki; Jumanne na Alhamsi,” akasema Bw Poghisio ambaye ni Seneta wa Pokot Magharibi.

Hoja hiyo iliungwa mkono kwa kauli moja na maseneta wa mirengo yote miwili.

Kenya imekuwa ikiandikisha idadi ndogo ya visa vya maambukizi ya virusi vya corona tangu mwishoni mwa wiki jana. Mnamo Jumanne ni visa 96 vipya pekee vilivyokanikiliwa kutoka na sampuli 3, 062 zilizopimwa ndani ya saa 24.