MakalaSiasa

Mabwanyenye wa Ukambani mbioni kupimana ubabe

September 5th, 2020 2 min read

KITAVI MUTUA na PIUS MAUNDU

SIASA za Ukambani zinaendelea kuchukua mwelekeo mpya huku uhasama mkubwa ukiibuka kati ya mabwenyenye wawili wakuu wanaounga Naibu Rais Dkt William Ruto kwa upande moja na kigogo wa siasa za eneo hilo Kalonzo Musyoka.

Bwanyenye Peter Muthoka na aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama mwenye mfuko mzito, sasa wanarindima ngoma ya Bw Musyoka na Dkt Ruto mtawalia, wakilenga kudhibiti siasa za eneo hilo.

Matajiri hawa wawili wamekuwa wakimwaga fedha ili kuamua mkondo wa siasa za Ukambani.

Kuingia kwa Bw Muthoka kwenye siasa za Ukambani kunaonekana kumkasirisha Bw Muthama ambaye alikuwa mfadhili mkubwa wa chama cha Wiper kabla ya uchaguzi wa 2017 na sasa amejitenga na mrengo huo wa Bw Musyoka.

Katika uchaguzi wa 2017, Bw Muthoka aliunga mkono mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto huku Seneta Muthama akivumisha injili ya kigogo wa ODM Raila Odinga na Bw Musyoka.

Hata hivyo, sasa mambo yamebadilika, Bw Muthoka akihamia upande wa Musyoka huku Seneta Muthama akipata hifadhi kwenye kambi ya Naibu Rais.

Mapema mwaka jana, Bw Muthoka aliandaa mkutano wa viongozi wote kutoka Ukambani katika hoteli ya Stoni Athi ambao ulihidhuriwa na wabunge 24, maseneta na magavana wote wa Ukambani pamoja na Bw Musyoka.

Hata hivyo, Bw Muthama hakuhudhuria mkutano huo wala sherehe za Krismasi katika Shamba la Bw Musyoka la Yatta ambao ulihudhuriwa na Bw Muthoka ambapo wanasiasa hao walipokezwa kitita kizito baada ya kukamilika kwake.

Bw Muthoka ni tajiri mkubwa anayemiliki kampuni ya Acceler Global Logistics inayohusika na usafirishaji wa bidhaa.

Naye Bw Muthama anashiriki kwenye biashara ya madini.Kinyume na Bw Muthama ambaye ni mkakamavu na hutoa cheche kali kwenye mikutano ya kisiasa, Bw Muthoka ni mpole sana na ni nadra sana aonekane akihudhuria wala kuhutubu kwenye mikutano ya kisiasa.

Huku uchaguzi mkuu wa 2022 ukikaribia, mabwenyenye hao wawili wanashiriki ubabe wa kuamua mwaniaji ambaye atanufaikia kura milioni mbili na zaidi za Ukambani.

Katika uchaguzi wa 2017, Bw Muthoka aliwafadhili wawaniaji wa Jubilee Ukambani kulikokuwa ngome ya kisiasa ya Muungano wa NASA. Alisaidia chama hicho kutwaa viti vitatu vya ubunge Ukambani.

Kwa sasa Bw Muthoka ndiye mshirika mkuu wa Rais Kenyatta eneo hilo huku akiaminika kusukuma ajenda ya kuhakikisha Bw Musyoka anakuwa rais 2022.

Bw Muthama naye ameahidi kuvumisha uwanizi wa Dkt Ruto eneo la Ukambani na maeneo mengine ya nchi.

Kwenye mahojiano na Taifa Jumapili, Bw Muthoka alikiri kwamba alihusika pakubwa kuhakikisha kwamba Wiper inaingia kwenye mkataba wa kisiasa na Jubilee.

“Wakati wa uchaguzi wa marudio 2017, Bw Musyoka alikuwa Ujerumani akimshughulikia mkewe aliyekuwa mgonjwa. Hata hivyo, alipiga simu na kuwaamuru wananchi wasusie uchaguzi wa pili licha ya kikosi changu kuendesha kampeni kali mashinani ili raia washiriki kura hiyo,” akasema Bw Muthoka.

Kwake, hiyo ilikuwa ishara ya kutosha kwamba Bw Musyoka ndiye kigogo wa siasa za eneo hilo ndiyo maana alimfikia baada ya kura hiyo kumshawishi ashirikiane na Jubilee ili kunufaisha jamii hiyo kwenye utawala wa sasa.

“Kuna watu wanaoshangaa kwa nini najihusisha na siasa ilhali mimi ni mfanyabiashara. Nafanya kwa manufaa ya jamii yangu,” akasema.

‘Tutaendelea na majadiliano na ni vyema ifahamike kwamba tushapiga hatua nzuri hasa na majirani wetu kutoka Mlima Kenya ambao wana kura nyingi mno. Bado tutaendelea na sitakimya Wakamba wakielekezwa visivyo kisiasa,’ akasisitiza.

Bw Muthoka ndiye alikuwa Mwenyekiti wa kamati ya kujadili ushirikiano kati ya Wiper na Jubilee.? Upande wa Wiper ulihusisha Maseneta Boniface Kabaka (Machakos), Enock Wambua (Kitui) na Mutula Kilonzo Jnr ( Makueni).

Jubilee nao waliongozwa na Spika Justin Muturi, Naibu Mwenyekiti David Murathe na Njee Muturi.

Juhudi za Bw Muthama za kumtaka Bw Musyoka aunde muungano na Dkt Ruto nazo zimekosa kutia baada ya Makamu huyo wa Rais wa zamani kuegemea mrengo wa Rais.