Habari

Mabwanyenye warudisha Sh1 trilioni walizokuwa wameficha ughaibuni

May 21st, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

WAKENYA matajiri wamerudisha nchini zaidi ya Sh1 trilioni, walizokuwa wameficha nje ya nchi.

Wananchi hao walifanya hivyo katika muda wa miaka mitatu iliyopita, baada ya kuondolewa adhabu na Hazina ya Fedha.

Wakati wa msamaha huo, Wakenya hao hawakuhitajika kuelezea kiini cha pesa hizo au kuelezea ushuru waliokwepa miaka iliyotangulia.

Msamaha huo ulitolewa na Waziri wa Fedha Henry Rotich mwaka wa 2016 na muda wake unakamilika mwezi ujao.

Mamlaka ya Kukusanya Ushuru (KRA) ilisema fedha hizo zilirudishwa na Wakenya 16,000 waliotuma maombi.

“Tumepokea maombi zaidi ya 16,000 na kufikia sasa Sh1,014,058,103,551. Hatua hiyo ililenga kuwatia moyo wananchi kurudisha mali nchini ili kuimarisha maendeleo,” ilisema KRA katika tangazo.

Pesa zilizorudishwa ni zaidi ya thuluthi moja ya bajeti ya humu nchini. Wakenya wengi matajiri uhifadhi mali yao mataifa ya ng’ambo kuepuka kulipa ushuru, au kuwekeza katika mataifa yaliyo imara.

Ripoti iliyochapishwa na taasisi ya utafiti ya Marekani ya National Bureau of Economic Research (NBER) mwaka 2018 ilionyesha kuwa wananchi matajiri kupindukia walikuwa wameshikilia zaidi ya Sh5 trilioni katika akaunti nje ya nchi ili kuepuka ushuru.

Ripoti nyingine iliyotolewa 2007 ilielezea jinsi watu wafisadi wakati wa uongozi wa Rais Mstaafu Daniel arap Moi walivyoiba takriban Sh130 bilioni na kuficha fedha hizo katika benki nje ya nchi, ikiwemo ni pamoja na Uingereza na Afrika Kusini.