HabariSiasa

Mabwawa: Hatua ya Rais yachemsha ngome ya Ruto

September 19th, 2019 2 min read

EVANS KIPKURA Na STANLEY KIMUGE

VIONGOZI wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet, wamemlaumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kufutilia mbali ujenzi wa bwawa la Kimwarer, eneobunge la Keiyo Kusini

Wakiongozwa na Seneta wa kaunti hiyo, Kipchumba Murkomen, viongozi hao walisema kwamba hatua ya Rais Kenyatta ya kufutilia mbali ujenzi wa bwawa hilo iliyotarajiwa kugharimu Sh22.2 bilioni ni sawa na kuadhibu wakazi kwa makosa yaliyofanywa na watu wengine.

Rais Kenyatta alichukua hatua hiyo baada ya kupokea ripoti kutoka kwa kamati ya kiufundi aliyoteua baada ya ujenzi wa bwawa hilo kuzua utata.

Bw Murkomen alilaumu kamati hiyo kwa kumpotosha rais ilipopendekeza kandarasi ifutiliwe mbali. Kulingana na Bw Murkomen, kamati hiyo ilitekeleza majukumu yake kwa ubaguzi.

“Kama vile ambavyo nimekuwa nikisema wakati huu wote mpango umekuwa ni kuua miradi hii. Kamati ilivyoundwa, haikuwa na usawa wa kijamii na kimaeneo. Watu wa Elgeyo Marakwet wamenyimwa haki yao ya miradi ya kitaifa kupitia vitendo vya ubaguzi makusudi,” alisema Bw Murkomen, ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika Seneti.

Alisema kamati hiyo haikushirikisha umma kabla ya kufikia uamuzi wake.

Rais Kenyatta aliruhusu ujenzi wa bwawa la Arror eneo la Marakwet Mashariki licha ya kukumbwa na madai ya ufisadi sawa na Kimwarer.

Maeneo hayo yako katika eneo la Rift Valley ambayo ni ngome kuu ya kisiasa ya Naibu Rais, Dkt William Ruto.

Mbunge wa Keiyo Kusini, Bw David Rono, ambako bwawa la Kimwarer lilipaniwa kujengwa alisisitiza kuwa wataendelea kushinikiza lijengwe.

“Tunataka kumshukuru Rais kwa kuruhusu ujenzi wa bwawa la Arror kuanza lakini tutaendelea kushinikiza ujenzi wa bwawa la Kimwarer uendelee pia. Tunajua kwamba kumekuwa na changamoto lakini tutamuomba aruhusu mradi huo kuendelea,” alisema Bw Rono.

Aliendelea: “Mradi huo ulikuwa wa kunufaisha jamii za Tugen na Keiyo. Tunahisi tumekosewa na tunaamini rais hakuelezwa ukweli. Nitaongoza ujumbe kumuomba abatilishe uamuzi huo,”alisema mbunge huyo.

Bw Rono aliongeza kuwa miradi hiyo miwili haitafaidi kaunti hiyo pekee bali nchi nzima kupitia nguvu za umeme.

Katika ripoti yake, kamati ya kiufundi ilisema bwawa la Kimwarer halikufaa kujengwa na kwamba gharama ya ujenzi iliwekwa juu kuliko inavyostahili.

Kamati ilisema iligundua kuwa hakukuwa na utafiti wa hivi punde kubaini ikiwa bwawa hilo lilifaa kujengwa.

Utafiti wa pekee kuhusu mradi unaofanana na ujenzi wa bwawa hilo ulifanywa miaka 28 iliyopita na uligundua kuwa mawe katika eneo hilo hayangeweza kustahimili bwawa lililonuiwa kujengwa.

Kiongozi wa chama cha ODM, kaunti ya Elgeyo Marakwet, Bw Micah Kigen, alisema ripoti ya kamati ya kiufundi ilijaa ubaguzi akisema utafiti ulifanywa na serikali ya Israel mwaka wa 1979 na kugundua kuwa mradi huo ungebadilisha maisha ya wakazi wa bonde la Kerio.

Bw Kigen aliungana na Bw Rono kusema kuwa wataomba rais kubadilisha uamuzi wake.

“Tutaomba uamuzi huu ubatilishwe kwa sababu ni ubaguzi unaolenga kuadhibu jamii ya Keiyo. Mradi huu ungesaidia watu zaidi ya 30,000 kuwekeza katika kilimo,” alisema.