Habari

Macharia kufika mbele ya PAC kujibu kuhusu kupotea kwa Sh60 bilioni

September 25th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Uchukuzi na Miundomsingi James Macharia na aliyekuwa Katiba wa Wizara hiyo John Mosonik wameitwa kufika mbele ya wabunge kujibu maswali kuhusu kupotea kwa Sh60 bilioni katika wizara hiyo katika mwaka wa kifedha wa 2016/2017.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC) Opiyo Wandayi alitangaza hayo Jumanne huku wanachama wa kamati hiyo wakipendekeza kuwa ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ifanya ukaguzi wa kipekee kwa akaunti za wizara hiyo katika kipindi hicho.

Katika mkutano na Katibu wa Wizara hiyo Profesa Paul Maringa, wanachama wa kamati hiyo walisema haitakubalika kwa wizara hiyo kufeli kuajibikia pesa ambazo ilipokea kutoka kwa Hazina ya Kitaifa.

“Baada ya kusikiza yale umesema, sidhani tutapata ukweli kuhusu suala hili ambalo lilianza mwaka 2017. Kama kamati sharti tuchukue hatua kali na hii ndiyo maana tunataka Waziri Macharia na aliyekuwa Katiba wake Bw Mosonik, na aliyekuwa Afisa wa Fedha kufika hapa kuangazia ukweli kuhusu kupotea kwa fedha hizi,” akasema Bw Wandayi ambaye ni Mbunge wa Ugunja.

Kulazimisha

Alisema kamati ya PAC ina mamlaka sawa na ya Mahakama Kuu na inaweza kuwalazimisha mawaziri na makatibu wa wizara kufika mbele yake kutoa maelezo kuhusu matumizi ya fedha za umma.

Kulingana na Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM act), shughuli zote za matumizi ya fedha za serikali zinafaa kunakiliwa katika Mfumo wa Usimamizi wa Kifedha kidijitali (IFMIS).

Bali hitaji hili halikuzingatiwa na Idara ya Miundomsingi katika Wizara hiyo kama ambavyo Profesa Maringa aliwaambia wabunge.

Katika utendakazi wake, ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu za serikali hutumia mfumo wa IFMIS kufuatilia matumizi ya fedha za umma.