Machifu kuaga afisi za kikoloni

Machifu kuaga afisi za kikoloni

Na MAUREEN ONGALA

KWA zaidi ya miaka 60, machifu katika eneobunge la Ganze wamekuwa wakitumia ofisi zilizojengwa na mkoloni.

Baadhi ya majengo hayo ni magofu na hatari kwa maisha kwani yanaweza kuporomoka wakati wowote.

Hali hii imewalazamu machifu hao kuwahudumia wananchi chini ya miti mara kwa mara ambapo huwa wanatatizwa na hali ya hewa.

Matatizo hayo huenda sasa yakasahaulika hivi karibuni baada ya Hazina ya Kitaifa ya Kustawisha Maendeleo katika Maeneo Bunge (NG-CDF) kuanzisha rasmi zoezi la kuwajengea machifu na manaibu wao ofisi.

Chifu wa lokesheni ya Mrima wa Ndege, Bw Samson Chai alisema kuwa ukosefu wa ofisi umemlazimisha kuzunguka vijijini anapotaka kuwahudumia wakazi.

Bw Chai alisema kuwa wengi wa wakazi wa eneo hilo wanajua kuwa hana ofisi na kwa hivyo humsimamisha popote pale watakapomwona ili awahudumie.

“Imekuwa changamoto kubwa sana kufanya kazi bila ofisi. Sehemu hii imejaa mchwa na imekuwa hatari kuweka stakabadhi katika chumba cha tope. Huwa inabidi kutembea nazo ndani ya mkoba,” akasema.

Alisema imekuwa changamoto pia kuwapa ujumbe muhimu wakazi kwa sababu ya kukosa ukuta wa kubandika mabango na ilani muhimu kutoka kwa serikali.

Mbunge wa Ganze, Bw Teddy Mwambire alichimba msingi wa ujenzi wa ofisi za chifu wa kata ya Kauma katika wadi ya Jaribuni na ile ya Mrima wa Ndege katika wadi ya Sokoke kuashiria mwanzo mpya kwa mazingara ya kikazi kwa machifu.

Akizungumza na wanahabari Bw Mwambire alisema machifu ni wawakilishi wa rais nyanjani na ni aibu wanapofanya kazi katika mazingira duni.

“Ofisi hizi za kisasa ni za kwanza kujengwa tangu wakati Kenya ilipopata uhuru eneo hili na pesa kwa serikali kwa sababu ofisi nyingi katika eneobunge la Ganze zimekuwepo tangu mwaka wa 1952,” akasema.

“Machifu hawana mahali pa kuweka stakabadhi na kila asubuhi wanatoka nyumbani kwao wakiwa wamebeba kiti na mkoba wakielekea chini ya mti. Inakuwa hatari wakati wa mvua kwani stakabadhi hizo zitaharibika,” akaongeza.

Bw Mwambire alisema kuwa eneobunge lake lina lokesheni 16 na kata ndogo 47.

Alieleza kuwa ndani wa mwaka huu wa kifedha NG-CDF itatumiwa kujenga ofisi sita za machifu wa Kauma, Mrima wa Ndege, Bamba na nyingine tatu ambazo hakutaja.

Bw Mwambire alisema kuwa anatarajia kuwa huenda eneobunge la Ganze likawa na lokesheni nyingine zaidi kufuatia ongezeko ya idadi ya watu katika maeneo tofauti.

“Kuna maeneo ambayo watu wamekuwa wengi na ili kupata hufuma bora ni lazima kuwe na viwango ambavyo vinastahili kuwa katika sehemu zile. Tunajipanga kuona ya kuwa tunaendeleza ujenzi wa shule, vituo vya polisi na afisi nyingine za utawala,” akasema.

You can share this post!

Phil Foden kukosa mechi tatu za kwanza za Manchester City...

DIMBA PWANI: Ilianza kama Action Boys FC, sasa ni Beach Bay...