Habari Mseto

Machifu, wahubiri walaumiwa kwa mauaji ya wazee

January 20th, 2020 1 min read

Na MAUREEN ONGALA

MACHIFU na wahubiri wamelaumiwa kwa mauaji ya wazee wanaodaiwa kuwa wachawi katika Kaunti ya Kilifi.

Mwenyekiti wa kituo cha kuokoa wazee wanaoshukiwa kuwa wachawi cha Kaya Godoma, Bw Emmanuel Katana amelalamika kuwa machifu wanachangia mauaji hayo kwa kutatua kesi kiholela bila kutoa suluhisho wakati wazee wanapowaendea kuomba msaada.

“Chifu anafaa kuwa mtu wa kwanza kulinda wazee dhidi ya mauaji. Badala yake huwa wanaweka vikao vya kujadili masuala hayo lakini hawatoi suluhisho, bali huwaambia wahusika waende wakasikizane wenyewe,” akasema Bw Katana.

Akizungumza wakati wa kuadhimisha miaka 10 tangu kituo hicho kilipoanzishwa, Bw Katana alisema hatua hiyo huwaacha wazee hao bila pa kukimbilia.

Bw Katana alisema chifu anaposhindwa kutoa mwelekeo kuhusu kesi inayopelekwa kwake huwa inaonekana kama kwamba tayari amemhukumu mshukiwa na kumwacha mikononi mwa watu wanaotaka kumuua.

“Tumekuwa na visa ambapo machifu wana mapendeleo wanapoendesha kesi hizo na hupendelea walalamishi,” akasema.

Alilaumu pia wahubiri ambao hudai wana uwezo wa kutabiri, kwani wao ndio husababisha uhasama katika familia na kuleta mauaji.

Kulingana na Bw Katana, wagonjwa wengi ambao hawajaenda kutafuta matibabu hospitalini huamua kwenda kufanyiwa maombi makanisani ambapo wanaambiwa kuwa wamerogwa.

“Unapomwambia mgonjwa aliyekosa matumaini kwamba amerogwa na babake, basi maisha ya mtu asiye na hatia yanawekwa hatarini. Familia huanza kutafuta njia za kuchangisha pesa ili kukodisha wauaji,” akasema.

Alieleza kuwa mienendo ya machifu imeathiri sana uwezo wa kuwakamata watu wanaotishia maisha ya wakongwe.

Kituo cha Kaya Godoma kilichoko katika kata ya Mrima wa Ndege, eneobunge la Ganze kilianzishwa mnamo 2008 na marehemu Emmanuel Kenga.