Michezo

Macho kwa Arsenal na Manchester City EPL ikichacha

May 4th, 2024 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA:

VIONGOZI Arsenal na nambari mbili Manchester City wanaalika Bournemouth na Wolves mtawalia, kila mmoja akitegea mwenzake ateleze ili abaki farasi wa pekee kwenye vita vinavyochacha vya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu (EPL).

Arsenal watalenga kusalia kileleni kwa kulipua nambari 10 Bournemouth ugani Emirates nao mabingwa watetezi City wako nyumbani Etihad dhidi ya nambari 11 Wolves.

Wanabunduki wa Arsenal wanajivunia rekodi nzuri dhidi ya Bournemouth ya ushindi mara nane, sare moja na kupoteza mara moja katika mechi 10 zilizopita.

Vijana wa kocha Mikel Arteta wanafukuzia ushindi wa tano mfululizo dhidi ya Bournemouth.

Katika mkondo wa kwanza ugani Vitality mwezi Septemba 2023, Arsenal walitwaa ushindi wa 4-0 baada ya kuona lango kupitia kwa Bukayo Saka, Martin Odegaard, Kai Havertz na Ben White.

Safari ya mwisho ya Bournemouth ugani Emirates pia iliishia kuwa kichapo cha 3-2 ambapo wageni waliongoza 2-0 dakika 45 za kwanza kupitia magoli ya Philip Billing na Marcos Senesi, kabla ya Arsenal kujibu kupitia Thomas Partey, White na Reiss Nelson kipindi cha pili.

Arsenal wameshinda michuano minne kati ya tano wamesakata Emirates mwaka huu, ingawa walionyesha wao pia wana udhaifu walipoaibishwa 2-0 na Aston Villa mnamo Aprili 14.

Bournemouth wanafukuzia ushindi wa tatu mfululizo msimu huu baada ya kupangua Wolves 1-0 na Brighton 3-0 katika mechi mbili zilizopita, kwa hivyo si wakudharauliwa.

Macho yatakuwa kwa Saka (Arsenal) na Dominic Solanke (Bournemouth).

Ugani Etihad, Man-City walichabanga Wolves mara mbili mfululizo, wanawinda ushindi wa tatu.

Vijana wa kocha Pep Guardiola hawajapoteza ligini tangu kichapo cha 1-0 kutoka kwa Villa mnamo Desemba 6, 2023.

Mara ya mwisho Wolves walizuru Etihad walizamishwa na mfumaji matata Erling Haaland 3-0 mnamo Januari 22, 2023.

Hata hivyo, Wolves waling’ata City 2-1 ugani Molineux walipokutana mapema msimu huu.

Mshambulizi Phil Foden pamoja na beki Ruben Dias walikosa mechi ya wikendi iliyopita wakiwa wagonjwa, lakini wanatarajiwa kurejea ulingoni kupiga jeki Man-City.

Naye Hwang Hee-chan ataongoza mashambulizi ya Wolves.

Upande wa chini za jedwali ‘malaria’ ya kushushwa ngazi yanaandama Nottingham Forest, Luton Town na Burnley katika nafasi ya 17 hadi 19, mtawalia.

Forest wako Sheffield United ambao shughuli wamebaki nayo ni kukamilisha ratiba kwa sababu wameshatemwa.

Ni fursa nzuri kwa wanamisitu hao kujinasua, hasa kwa sababu Burnley wana kibarua kigumu dhidi ya mabwanyenye Newcastle (nambari saba) wanaotafuta kuingia mduara wa kushiriki mashindano ya Ulaya.

Wakati huo huo, wenyeji Chelsea walikuwa wembe wakivuruga juhudi za Tottenham Hotspur kurukia nafasi za kuingia Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), walipowatitiga 2-0 ugani Stamford Bridge mnamo Alhamisi usiku.