Michezo

Macho kwa Olunga ambaye ni mwiba kwa DRC

June 15th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Harambee Stars imewasili jijini Madrid nchini Uhispania tayari kuendeleza ubabe dhidi ya Jamhuri ya Kidemkrasia saa mbili usiku Juni 15 katika mechi yake ya mwisho kabla ya kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri litakaloandaliwa Juni 21 hadi Julai 19, 2019.

Stars ya kocha Sebastien Migne ilinyuka Leopards ya Florent Ibenge 2-1 zilipokutana mara ya mwisho uwanjani Kenyatta mjini Machakos mnamo Machi 26, 2017.

Mshambuliaji wa Keshiwa Reysol, Michael Olunga alifunga mabao yote mawili akicheka na nyavu dakika ya sita na 71, huku Gael Kakuta akipachika bao la DR Congo kufutia machozi dakika ya 60.

Ushindi huo ulikuwa wa pili mfululizo dhidi ya DR Congo baada ya kuwalima 1-0 kupitia bao la Olunga mnamo Oktoba 4, 2016 jijini Kinshasa.

Mara ya mwisho Kenya ilipoteza dhidi ya DR Congo ilikuwa 1-0 Januari 17, 2011.

Ilichapwa 1-0 mara mbili mwaka huo, huku kipigo chake cha kwanza kikiwa Januari 8, 2011. Mechi zote ambazo mataifa haya yamekutana ni za kirafiki.

Kenya itarejea jijini Paris mapema Jumapili na itaelekea nchini Misri mnamo Juni 19. Italimana na Algeria (Juni 23), Tanzania (Juni 27) na Senegal (Julai 1) uwanjani 30 June jijini Cairo.

Huku Kenya inayojivunia kuwa na nyota Victor Wanyama kutoka Tottenham Hotspur ikijiandaa kwa mtihani wa DR Congo, majirani wake Uganda Cranes wametuma onyo kwa wapinzani wake wa Kundi A Misri, DR Congo na Zimbabwe kwa kuchabanga Ivory Coast 1-0 Juni 15.

Farouk Miya amepachika penalti iliyozamisha Elephants ya Ivory Coast katika dakika ya 35 jijini Abu Dhabi nchini Milki za Kiarabu. Nayo Black Stars ya Ghana na Bafana Bafana ya Afrika Kusini zimetoka 0-0.