Kimataifa

Macho kwa Refa Mkenya ‘kuamua’ mechi kati ya Morocco na DR Congo

January 21st, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

MWAMUZI Mkenya Peter Waweru Kamaku atashika kipenga leo Jumapili, Januari 21, 2024 katika mechi kati ya Morocco na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) kwenye kipute cha Dimba la Kandanda la Mataifa ya Bara Afrika (AFCON 2023) kinachoendelea nchini Ivory Coast.

Kamaku anarejea kutoa maamuzi katikati ya uga baada ya kushiriki makala ya AFCON yaliyopita ya 2021 nchini Cameroon.

Tayari mwamuzi huyu ameshiriki mechi ya AFCON 2023 baada ya kuwa refa msaidizi wa video (VAR) Mozambique ilipokabana koo na Misri mchuano wa Kundi la B.

Soma pia https://taifaleo.nation.co.ke/michezo/cape-verde-watandika-msumbiji-na-kudhibiti-kilele-cha-kundi-b-katika-afcon

Kamaku aliangaziwa sana baada ya kuwapa Mafarao mkwaju wa penalti dakika za lala salama na wakavunja nyoyo za Mambas mechi ikiishia sare ya 2-2.

Mshambulizi wa Misri Mohamed Salah alitia kimiani mpira baada ya adhabu kutolewa Domingos Macandza alipomwangusha Mostafa Mohamed katika kisanduku.

Soma pia https://taifaleo.nation.co.ke/michezo/afcon-senegal-wakomoa-cameroon-na-kutinga-hatua-ya-16-bora

Waweru atasimamia toleo la tatu la AFCON mfululizo baada ya kushiriki mara ya kwanza 2019 nchini Misri.

Atakuwa mwamuzi katika uga wenye uwezo wa kubeba mashabiki 20,000 wa Stade Laurent Pokou eneo la San Pedro, Ivory Coast.

Mtanange kati ya Mabingwa mara mbili DRC (1968 na 1974) na bingwa mara moja Morocco (1976) utagaragazwa saa kumi na moja jioni.

Afcon 2023 ni Makala ya 34 tangu mchuano huo wa Bara Afrika uzinduliwe na Muungano wa Soka Afrika.