Michezo

Macho yote kwa Conseslus mbio za mita 3000 kuruka viunzi

October 1st, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA watafuatilia matokeo ya Conseslus Kipruto kwa makini atakapoongoza Benjamin Kigen, Abraham Kibiwot na Leonard Bett katika kampeni za kufuzu kushiriki fainali ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Riadha za Dunia jijini Doha nchini Qatar, leo Jumanne jioni.

Kipruto hajawa na mwaka mzuri, ingawa anajivunia kushindia Kenya dhahabu katika Olimpiki (2016), Dunia (2017), Jumuiya ya Madola (2018) na Afrika (2018).

Alipata tiketi ya moja kwa moja kutetea taji kwa kuwa aliibuka mshindi jijini London nchini Uingereza miaka miwili iliyopita.

Licha ya kuwa na msimu mbaya, Conseslus bado anaaminiwa na Wakenya. Hata hivyo, bingwa wa michezo ya Afrika mwaka 2019 Kigen, mshindi wa Riadha za Afrika za chipukizi mwaka 2015 Kibiwot na bingwa wa Riadha za Dunia za chipukizi mwaka 2017 Bett watalazimika kutomtegemea sana wakitafuta kuendeleza ubabe wa Kenya.

Kenya ilishinda makala sita yaliyopita kupitia kwa Brimin Kipruto (2007), Ezekiel Kemboi (2009, 2011, 2013 na 2015) na Conseslus (2017).

Hata hivyo, utawala huu wake utakuwa hatarini jijini Doha, hasa baada ya Mmoroko Soufiane El Bakkali kushinda duru tatu kati ya sita kwenye Riadha za Diamond League mwaka 2019.

Raia wa Ethiopia, Waganda na Waamerika ni baadhi ya wakiambiaji wanaotarajiwa kutoa upinzani mkali kwa Wakenya katika makala haya.

Rotich

Naye Ferguson Rotich anabeba matumaini yote ya Kenya kupata medali katika mbio za mita 800 za wanaume, leo Jumanne usiku.

Hii ni baada ya wawakilishi wengine Emmanuel Korir na Ng’eno Kipng’etich kubanduliwa nje katika nusu-fainali Jumapili usiku.

Korir na Kipng’etich walimaliza nusu-fainali katika makundi yao katika nafasi ya tatu na sita, mtawalia.

Kundi la kwanza lilikuwa na kasi ya juu kwa hivyo watimkaji wanne, tofauti na wawili kutoka kundi la pili na tatu, waliingia fainali.

Rotich alikamilisha kundi la kwanza katika nafasi ya pili kwa dakika 1:44.20 nyuma ya raia wa Puerto Rico Wesley Vazquez (1:43.96).

Mkenya huyu mwenye umri wa miaka 28 atalazimika kujitahidi katika mbio hizi za kuzunguka uwanja mara mbili ili kuwa jukwaani kupokea medali.

Rotich anatafuta medali yake ya kwanza baada ya kuambulia pakavu katika makala matatu yaliyopita. Alivunja sheria ya kutoingia katika laini ya mkimbiaji mwingine katika ziara yake ya kwanza kwenye Riadha za Dunia mwaka 2013 jijini Moscow nchini Urusi.

Mwaka 2015 jijini Beijing nchini Uchina, Rotich alimaliza nafasi moja nje ya mduara wa medali kabla ya kushindwa kufika fainali mwaka 2017 jijini London nchini Uingereza.

Bingwa huyu wa Riadha za Diamond League mwaka 2016, ambaye msimu huu alivuna ushindi kwenye duru ya London mwezi Julai, atakabiliana na washiriki Marekani, Uhispania, Poland, Uingereza, Tunisia, Qatar na Puerto Rico katika fainali.

Hapo Jumapili, bingwa mara sita wa matembezi ya kilomita 20 barani Afrika, Grace Wanjiru alimaliza kampeni yake katika nafasi ya 26 kati ya washiriki 45 walioanza, kwa saa 1:39:58. Uchina ilifagia medali zote katika kitengo hiki kupitia kwa Hong Liu, Shenjie Qieyang na Liujing Yang.