Macho yote kwa Haji kuhusu wizi wa mabilioni Kemsa

Macho yote kwa Haji kuhusu wizi wa mabilioni Kemsa

Na ANGELA OKETCH

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Noordin Haji anasubiriwa kwa hamu kuwachukulia hatua waliohusika na kashfa ya uporaji wa mabilioni ya pesa iliyokumba mamlaka ya ununuzi na uuzaji dawa kwa hospitali za serikali (KEMSA) wakati wa ununuzi wa vifaa vya kupambana na ugonjwa hatari wa Corona.

Tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC) ilikamilisha uchunguzi wa kashfa hiyo na kumkabidhi DPP faili hiyo mnamo Oktoba 22, 2020 ili aitathmini na kutoa mwelekeo.

EACC ilichapisha ripoti kuhusu uchunguzi iliyofanya katika kashfa ya KEMSA. Katika ripoti hiyo, tume hii ya kupambana na ufisadi ilisema sheria za ununuzi wa bidhaa zilikiukwa.

Pia, EACC ilisema sheria kuhusu usimamizi na matumizi ya pesa za umma katika ununuzi na ulipaji huduma zilivunjwa kiholela na maafisa katika KEMSA mwaka uliopita. Kulingana na arifa iliyochapishwa na EACC uchunguzi ulibaini kuwa, bajeti iliyokuwa imetengewa KEMSA ilipita kwa takribani Sh3.2bilioni.

KEMSA , EACC ilisema ilitumia pesa zaidi kuliko kiwango kile ilikuwa imekubaliwa.

EACC ilisema mamlaka hiyo ya ununuzi wa dawa na bidhaa za hospitali haikueleza sababu za kuteua waliotoa huduma moja kwa moja badala ya kufanya mahojiano ndipo atakayehitimu ashinde zabuni ya kununua bidhaa zilizohitajika kupambana na mkurupuko wa ugonjwa huu wa Corona.

Hata hivyo shirika hilo lilijitetea wakati wa mahojiano kwamba, liliwajibika kununua bidhaa hizo kwa njia ya dharura.

Kulingana na ripoti hiyo ya EACC, waliopewa kandarasi kununua bidhaa hizo za kupambana na ugonjwa wa Covid-19 hawakuziwasilisha katika wakati zilipohitajika na kupelekea mamlaka hiyo kutumia vibaya pesa za umma.

“Bidhaa hizo zinarundikana katika maghala ya KEMSA,” ripoti hiyo ya EACC inasema.

Uchunguzi huo umesema kuwa, KEMSA haikunufaika na pesa ilizotumia kununua bidhaa hizo kwa bei ya juu kuliko vile zinauzwa zikitengenezewa humu nchini.

You can share this post!

Makahaba walilia serikali iwalinde dhidi ya dhuluma za...

Wahudumu wa afya wanunuliwa pikipiki kulinda wakazi dhidi...