Michezo

Macho yote kwa Kenya katika mbio za Valencia

October 2nd, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

Macho yatakuwa kwa Kenya wakati wa mbio za kilomita 42 na kilomita 21 za Valencia zitakazofanyika Desemba 6 nchini Uhispania ambako Wakenya watalenga kumaliza utawala wa Waethiopia.

Katika mbio za marathon, bingwa wa Boston na Chicago Marathon Lawrence Cherono atalenga kuwa Mkenya wa kwanza kutwaa taji baada ya Sammy Kitwara kufanya hivyo mwaka 2017 kabla ya Ethiopia kutawala makala mawili yaliyopita.

Mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 Joyciline Jepkosgei pamoja na mshikilizi wa rekodi hiyo sasa Peres Jepchirchir wako katika orodha ya kinadada wanne kutoka Kenya watakaowania umalkia wa kilomita 42 mjini Valencia.

Bingwa wa kilomita 21 wa mbio za Cardiff, Berlin, Boston Prague na Kisii, Joan Chelimo pamoja na mshindi wa Ras Al Khaimah Half Marathon Fancy Chemutai wanakamilisha orodha ya Wakenya watakaotafuta kumaliza ukame wa miaka mitatu bila taji la Valencia Marathon.

Chemutai atakuwa akishiriki marathon kwa mara yake ya kwanza kabisa. Wakenya hao watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Waethiopia Ruti Aga, Birhane Dibaba, Zeineba Yimer, Tigist Girma na Mare Dibaba na Muamerika Jordan Hasay wanaojivunia muda bora.

Orodha ya wanaume kutoka Kenya wanaoshiriki mbio za kilomita 21 inajumuisha Stephen Kiprop, Bedan Karoki, Bernard Ngeno, Alexander Mutiso, Philemon Kiplimo, Geoffrey Koech, Alfred Barkach, Kelvin Kiptum, William Wanjiku na chipukizi matata Rhonek Kipruto ambaye ameingia nusu-marathon kwa mara ya kwanza kabisa. Muethiopia Yomif Kejelcha hatetei taji lake.

Jepkosgei alikuwa Mkenya wa mwisho kushinda mbio za kilomita 21 za Valencia za wanawake mwaka 2017 alipozikamilisha kwa rekodi ya dunia ya saa 1:04:51.

Muethiopia Senbere Teferi alishinda kitengo hicho kwa saa 1:05:32 mwaka 2019.  Wapinzani wake wakuu ni Emily Sisson (Amerika), Sheila Chepkirui (Kenya), Charlotte Purdue (Uingereza) na Muethiopia Letesenbet Gidey ambaye anapanga kujitosa katika nusu-marathon siku hiyo.