Habari

Machungu ambayo Wakenya watapitia kufadhili bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2020/21

June 11th, 2020 3 min read

Na CHARLES WASONGA

HUKU Wakenya wengi wakiendelea kukabiliwa na hali mgumu kwa kupoteza ajira kutokana na janga la Covid-19, huenda wakakabiliwa na changamoto nyingine ya kupanda kwa bei ya bidhaa za kimsingi na kodi ya nyumba.

Hii ni kutokana na hatua ya serikali kupendekeza kuongeza ushuru unaotozwa bidhaa za matumizi ya nyumbani kama vile chakula na gesi ya kupikia, kulingana na Mswada wa Fedha wa 2020.

Na gharama ya uzalishaji chakula itapanda baada ya serikali kupendekeza ushuru wa thamani (VAT), wa kiasi cha asilimia 14 kwa vifaa vya kilimo, kama vile trekta.

Japo hizi ni baadhi ya mbinu ambazo serikali inapanga kutumia kuiwezesha kupata fedha za kutekeleza Bajeti ya Sh2.7 trilioni iliyosomwa Alhamisi na Waziri wa Fedha Ukur Yatani, zinahujumu mipango yake chini ya Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.

Kulingana na bajeti hiyo ambayo ilisomwa bungeni Alhamisi, serikali inatarajiwa kukusanya Sh1.62 trilioni kutokana na ushuru lakini itatumia Sh904 bilioni kulipia madeni.

Na kwa kuwa serikali inapanga kutumia Sh1.8 trilioni kufadhili matumizi yake, hii ina maana kuwa kuna upungufu wa Sh600 bilioni katika bajeti hii.

Ushuru wa VAT unaopendekezwa kutozwa bidhaa za kimsingi kama vile mahindi, unga wa ngano, maziwa na mayai na vyakula vinginevyo utapandisha bei ya bidhaa hizo wakati huu mgumu. Wakati huu bidhaa hizi hazitozwi ushuru huo.

“Japo Mswada huo wa Fedha haujatoa ufafanuzi zaidi, bila shaka hatua ya kurejeshwa kwa ushuru wa VAT kwa bidhaa za vyakula itapandisha bei ya bidhaa hizi wakati huu ambapo mapato ya raia wengi yamepungua kutokana na janga la Covid-19,” anasema mtaalamu wa masuala ya uchumi Tony Watima.

Anaongeza kwa serikali kupanga kuanza kutoza ushuru wa asilimia 14 kwa bidhaa za kilimo kama vile trekta, gharama ya kilimo itapanda.

“Hii itaenda kinyume na azma ya serikali ya kufanikisha ajenda ya utoshelezaji wa chakula kufikia mwaka wa 2022,” Bw Watima anaeleza.

Na kulingana na mswada huo ambao uliwasilishwa bungeni mwezi jana, serikali inapendekeza kutoza ushuru wa VAT wa asilimia 14 kwa gesi ya kupikia, hatua ambayo itachangia kupanda kwa bei bidhaa hiyo.

Hii ina maana kuwa ikiwa wabunge watapitisha mswada huo bei kilo 6 ya gesi itapanda kutoka Sh1,000 hadi Sh1,060 jijini Nairobi, ishara ya kupanda kwa gharama ya maisha.

Vile vile, serikali inaonekana kwenda kinyume na mpango wake wa kuhakikisha uwepo wa nyumba za gharama ya chini, kwa kupendekeza kutoza ushuru watu wanaoweka akiba ya kununua nyumba.

Kufikia sasa zaidi ya watu 20,000 wameweka akiba ya zaidi ya Sh230 milioni chini ya mpango kwa jina “Boma Yangu” unaosimamiwa na Idara ya Nyumba.

Ikiwa wabunge watapitisha mswada huu zaidi 300,000 ambao wamejisajili kwa mpango huu watavunjika moyo, kwani itawachukua muda mrefu kuweka akiba ili waweze kununua nyumba.

Mswada huo pia unapendekeza kuongeza ushuru unaotozwa mapato kutokana na nyumba za kukodisha kutoka kima cha asilimia 10 hadi asilimia 15 kwa watu mapato ya Sh144,000 kwa mwaka kwenda juu.

Hii ina maana kuwa wamiliki wa nyumba za makazi, na za kibiashara, watapandisha kodi.

Hazina ya kitaifa pia inalenga kutoza ushuru wa mapato wa kima cha asilimia 25 kutokana na pensheni inayolipwa wazee wenye umri wa miaka 65 pamoja na wafanyakazi wanaowasilisha michango yao kwa Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF).

Malipo ya wazee hawa huwa hayatozwi ushuru wa mapato ilivyo kwa watu wengine. Kwa hivyo, endapo mswada huo utapitishwa bila kufanyiwa bila kuondolewa kwa pendekezo hilo, itakuwa pigo katika juhudi za serikali za kuwafaa wazee hawa wakatu huu wa janga la Covid-19.

Na watu wanaoendesha biashara mitandaoni wengi wao wakiwa vijana hawajasazwa kwani mapato yao yatatozwa ushuru wa asilimia 1.5

Vidokezo

1: Vyakula kama unga, maziwa na mkate kutozwa ushuru wa VAT wa asilimia 14

2: Gesi ya kupikia kutozwa VAT ya asilimia 14

3: Trekta na vifaa vingine vya kilimo kutozwa VAT ya asilimia 14

4: Ushuru wa mapato ya nyumba wapandishwa kutoka asilimia 10

5: Akiba ya kununua nyumba kutozwa ushuru

6: Wazee kulipa ushuru wa asilimia 25 kwa pensheni

7: Wafanyabiashara mitandaoni kulipa ushuru wa asilimia 1.5 kwa mapato yao.