Habari Mseto

Mackenzie alishwa kizuizini kwa mfumo wa pasi ndefu

January 18th, 2024 1 min read

NA ALEX KALAMA

MAHAKAMA Kuu ya Malindi mnamo Jumatano iliarifiwa ya kwamba mhubiri tata Paul Mackenzie anayehusishwa na mauaji ya watu katika msitu wa Shakahola, alinyimwa chakula na maji kwa muda wa siku mbili zilizopita.

Akielezea mahakama mbele ya Jaji Mugure Thande, wakili Wycliffe Makasembo anayemwakilisha Mackenzie na wenzake 30 ambao wanatarajiwa kukumbana na mashtaka 191 ya mauaji yaliyotokea msituni Shakahola, aliiambia mahakama kuwa wateja wake wanapitia hali ngumu gerezani wanakozuiliwa.

“Nikiwa mbele ya mahakama hii naomba niweke wazi kwamba wateja wangu kwa muda wa siku mbili zilizopita hawajapewa chakula wala maji, akasema Bw Makasembo.

Aliiomba mahakama kuamuru usimamizi wa gereza wanakozuiliwa kuhakikisha wateja wake wanapewa chakula na maji badala ya kulishwa kwa mfumo wa pasi ndefu.

Jaji Thande alitoa agizo kwa usimamizi wa gereza ambalo Mackenzie na wanzake 30 wanazuiliwa kuhakikisha wanapewa chakula na maji kama inavyofanyika kwa wafungwa wengine.

Washukiwa hao watapelekwa hospitalini kupimwa akili.

Kesi hiyo itatajwa tena Febuari 6, 2024.

Inadaiwa Mackenzie alitumia kipaji chake cha ‘uhubiri’ kuwashawishi wafuasi wake kufunga hadi kufa ili “wakutane na Yesu”.