Kimataifa

Macron na Mattarella wa Italia kuzuru Kenya

December 10th, 2018 1 min read

Na Patrick Lang’at

RAIS wa Ufaransa Emmanuel Macron (pichani) na mwenzake wa Italia Sergio Mattarella ni miongoni mwa viongozi mashuhuri wa ulimwengu ambao watazuru nchini mapema mwaka 2019.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni Monica Juma alisema kwamba Rais Uhuru Kenyatta atakuwa mwenyeji wa viongozi hao Januari na Februari 2019. Bw Macron atakuwa akihudhuria kongamano la nne la Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira (UNEA-4) litakaloandaliwa Nairobi kati ya Machi 11 na Machi 15, 2019 jijini Nairobi.

Pia atakutana na Rais Kenyatta kwa mazungumzo ya kibiashara. Naye Rais Mattarella atazuru Kenya Februari. Dkt Juma aliambia Taifa Leo kwamba Kenya inatumia ziara hizo na zile za Rais Kenyatta katika mataifa mbali mbali kuimarisha ushirikiano na kutafuta sekta za kukuza ushirikiano zaidi.

Kenya imekuwa kivutio kikuu huku viongozi wa nchi mbali mbali wakiitembelea.

“Kile ambacho kimekuwa kikitendeka katika miezi kumi iliyopita ni kutaka kuhakikisha kila hatua inaleta faida na tumefanya hivyo maksudi,” Waziri Juma alisema.