Mada nzito Raila, Ruto wanakwepa

Mada nzito Raila, Ruto wanakwepa

Na LEONARD ONYANGO

VIGOGO wa kisiasa wanaopigania urais 2022, Naibu Rais William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga, wanaonekana kukwepa kimakusudi masuala nyeti yanayoathiri mamilioni ya Wakenya.

Badala yake, wawili hao wamekuwa wakizungumzia masuala kuhusu watakavyosaidia maskini kujinasua kutokana na hali zao za uchochole.Na wachanganuzi wa kisiasa wasema hatua hiyo ni ya kimakusudi.

“Wanasiasa watakuwa wanagusia hapa na pale masuala hayo lakini wanaogopa kufichuana kwa kuwa wote wana wapungufu yao.Hakuna mwaniaji wa urais yuko tayari kufichua mwenzake kuhusiana na unyakuzi wa ardhi ama ufisadi.

Akifichua yeye pia anafichuliwa kwa vile wote ni wahusika katika unyakuzi wa ardhi na ufisadi,” asema Profesa Macharia Munene, mhadhiri wa masuala ya siasa katika Chuo Kikuu cha United States International Africa (USIU), Nairobi.

Prof Macharia anasema suala kuu la kampeni ambalo litaangaziwa zaidi kwenye kampeni za 2022 ni uchumi: “Uchumi mbovu ndilo tatizo kuu linalohangaisha mamilioni ya Wakenya na wapigakura watachagua mwanasiasa atakayeelezea mikakati mwafaka ya kufufua uchumi.

”Wakili na mtaalamu wa masuala ya utawala, Javas Bigambo, anasema huenda masuala hayo yakaibuka uchaguzi ukikaribia.“Haya ni masuala ambayo hayataepukika kadiri Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao unapokaribia.

Hata Bw Raila na Dkt Ruto wakikwepa kuyazungumzia katika kampeni zao kwa sasa, masuala hayo yataibuliwa tu na itabidi watangaze msimamo wao,” anasema By Bigambo.Mdadidisi huyo asema kwamba, Dkt Ruto na Bw Odinga wanaogopa kuibua masuala hayo mapema ili yasije yakakosa mvuto uchaguzi ukikaribia.

Kwenye ahadi zao kuhusu kukweza maskini kiuchumi, wanasiasa hao hawajajitokeza wazi kufafanua watakavyotekeleza ahadi zao kifedha na kimikakati, ikizingatiwa matatizo ya kiuchumi yanayokumba taifa kwa sasa.

Kulingana na wachanganuzi wa uchumi, mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta atakabidhiwa nchi iliyosakamwa na changamoto za kiuchumi.Mwanauchumi Dennis Kabaara anasema atakayeingia Ikulu baada ya uchaguzi ujao atakumbana na matatizo kama Ajenda Nne Kuu zilizokwama, ugatuzi unaoyumba, madeni na miradi mikubwa iliyokwama.

Anasema hii italazimu atakayechukua usukani kuwaongezea wananchi ushuru ili kulipa madeni na mahitaji mengine ya kiserikali, hatua ambayo itaacha serikali yake bila pesa za kufadhili ahadi kama vile “Bottom Up” yake Dkt Ruto na Sh6,000 kila mwezi kwa watu maskini milioni mbili zinazopendekezwa na Bw Odinga.

Huku wakifahamu kuwa ahadi zao hazina mashiko, wawili hao wamesalia kimya kuhusu masuala yenye umuhimu zaidi kwa mwananchi wa kawaida kama vile ardhi, bei za juu za bidhaa msingi, uhaba wa kazi kwa vijana miongoni mwa mengine.

Tatizo la unyakuzi ardhi lilikuwa miongoni mwa masuala makuu yaliyotawala kampeni za urais za 2013 na 2017, ambapo Bw Odinga alitumia suala hilo kushawishi wakazi wa Pwani wasipigie kura Jubilee.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017, Rais Kenyatta alisalimisha ekari 2,000 kwa maskwota katika Kaunti ya Taita Taveta kama njia mojawapo ya kuvutia kura katika eneo la Pwani baada ya kukiri familia ya Kenyatta inamiliki ekari 30,000 eneo hilo.

Bw Odinga, hata hivyo, alishutumu hatua hiyo ya Rais Kenyatta akisema ekari 2,000 hazikutosha.Kwa upande wake, Bw Ruto amesalia kimya kuhusu utata wa mashamba Pwani na maeneo mengineyo ya nchi.

Wawili hao pia wanahepa kujadili jinsi wanavyopanga kupambana na ufisadi iwapo watachaguliwa, kutokana na kile wadadisi wanasema ni kukolea kwa ufisadi miongoni mwa washirika wao, huku wao pia wakihusishwa na baadhi ya kashfa kubwa kubwa za uporaji wa mali ya umma.

You can share this post!

Askofu aonya raia kuhusu wanasiasa kampeni zikianza

Mawaziri 4 wampuuza Naibu Rais

T L