Habari Mseto

Madai machifu wasukuma raia kutia saini BBI

December 2nd, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

Uadilifu wa mchakato wa kubadilisha katiba wa Mpango wa Maridhiano (BBI), umeanza kutiliwa shaka baada ya watu kulalamika kwamba wanashurutishwa na kutishwa kutia saini kuunga mswada huo.

Ripoti kutoka maeneo mbalimbali zilisema kwamba machifu na manaibu wao wamekuwa wakiwatisha watu kutia saini kuunga mswada huo.

Ingawa afisi ya kushirikisha mchakato huo inasema kwamba haitumii maafisa wa utawala katika ukusanyaji wa saini, makamishina wa kaunti wamekuwa msitari wa mbele kuongoza shughuli hiyo. Kufikia Jumatatu, afisi hiyo ilitangaza kuwa ilikuwa imekusanya zaidi ya saini 1.7 milioni, zikiwa ni zaidi ya zinazohitajika kuunga mswada wa kura ya maamuzi.

Saini hizo zilikusanywa ndani ya siku nne.

Ripoti kutoka maeneo mbalimbali zilisema kwamba machifu walikuwa wakiwashurutisha vijana wanaoshiriki mpango wa Kazi Mitaani kutia saini kuungwa mswada huo au wasimamishwe kazi.

Baadhi ya wafanyakazi wa umma pia walilalamika kuwa walilazimishwa kutia saini mswada huo

Machifu hao wakatakiwa kuwasilisha ripoti kwa makamishna wa kaunti ndogo ambao wanajumuisha idadi ya watu waliotia saini katika maeneo yao kabla ya kuziwasilisha kwa makamishna wa kaunti.

Wanaharakati wanasema hii inathibitisha mageuzi yanayokusudiwa sio ya umma inavyodaiwa mbali ni ya serikali.

“Machifu sio halali kwa sababu katiba ya 2010 ilipendekeza waondolewe na sasa wanatumiwa kulazimisha watu kushiriki mchakato haramu wa kugeuza katiba,” asema mwanaharakati Boniface Mwangi wa Vuguvugu la Linda Katiba.

Katika mitandao ya kijamii, Wakenya walilalamika kwamba wanashinikizwa kutia saini kuunga kura ya maamuzi ilhali hawajasoma mswada wenyewe. Kulingana na mbunge wa Marakwet Mashariki Kangongo Bowen wananchi wa kawaida wanatishiwa kutia saini kuunga mswada ambao hawajauona na kuukubali.

“Fomu ambazo machifu wanazungusha kulazimishwa watu kutia saini hazijaambatishwa na mswada wenyewe ili wasome na kukubaliana na yaliyomo,” alisema kwenye ujumbe wa Twitter.

Machifu ambao hawakutaka watajwe majina wakihofia usalama wao waliambia Taifa Leo kwamba wamepatiwa vitabu na idadi ya saini ambazo wanafaa kukusanya katika maeneo yao.

“Inategemea idadi ya watu katika eneo lako. Tumeagizwa kuhakikisha tumekusanya saini nyingi kabla ya muda wa wiki moja,” alisema chifu mmoja kaunti ya Machakos.

Hata hivyo, alikanusha madai kwamba wanawashurutisha watu kutia saini fomu hizo. Mhadhiri wa chuo kikuu cha Nairobi Wandia Njoya anasema kwamba kutumia vitisho kukusanya saini kunafanya mchakato huo kuwa haramu zaidi.

“Hatufai kukataa mswada huu kwenye kura ya maamuzi. Tunafaa kususia kura hiyo. Ikiwa wanatumia machifu, hakuna hakikisho kuwa matokeo ya kura hiyo yatakuwa ya haki,” alisema.

Kulingana na Bi Njoya, Wakenya wanalazimishwa kukubali mageuzi ya kikatiba.

Mnamo Jumatatu, Gavana wa Makueni aliwasisha ombi katika Mahakama ya Juu akitaka ufafanuzi kuhusu iwapo maafisa wa serikali wanafaa kuongoza mchakato wa kubadilisha katiba.

Hatua yake inajiri baada ya mashirika ya kijamii ya Kongamano la Mageuzi na vuguvugu la Linda Katiba kusistiza kuwa juhudi za kubadilisha katiba ni siri ya watu wawili ambao wanataka kutumia Wakenya kutimiza maslahi ya kibinafsi.

Wanaharakati na wataalamu wa katiba wanasisitiza kuwa kinachohitajika ni kutekeleza katiba ya 2010 kikamilifu na sio kuibadilisha.

Ingawa makamishna wa kaunti na machifu wameonekana wakiongoza ukusanyaji wa saini kote nchini, wenyeviti wenza wa afisi ya kushirikisha mchakato wa BBI Junet Mohamed na Dennis Waweru walidai maafisa hao wanadumisha usalama.