Habari MsetoSiasa

Madai ya 'Tangatanga' Joho analangua mihadarati ni upuuzi – Junet Mohamed

February 6th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa ODM Jumatano waliendelea kumtetea Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho baada ya wandani wa Naibu Rais William Ruto kumhusisha biashara za dawa za kulevya.

Wakiongozwa na kiranja wa wachache Junet Mohamed wabunge hao 11 walidai kuwa gavana wa Nandi Stephen Sang’, na wenzake, wanamshambulia Bw Joho kwa kukosa “kazi” baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutoa amri iliyowanyima nafasi ya kuandama na Bw Ruto kila mara wakizindua “miradi ghushi”.

“Hawa watu ambao ni wanachama wa “Team Tanga Tanga” wamekosa kazi ya kufanya ndio maana wameanza kumtusi Bw Joho kwa kudai yeye ni mlanguzi wa dawa za kulevya ilhali hawana ushahidi wowote kuthibitisha madai yao,” akasema.

Bw Mohammed ambaye ni mbunge wa Suna Mashariki alieleza kuwa hatua ya Rais Kenyatta ya kumtwika Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i wajibu wa kusimamia utekelezaji wa miradi ya serikali imewafanya wandani hao wa Dkt Ruto kukosa ajenda ya kuuza katika kampeni zao za uchaguzi wa 2022.

“Hii ndio maana wameanza kumshambulia Gavana Joho kwa sababu yeye ni tisho kwa ndoto za bosi wao,” akasema aliposoma taarifa kwa niaba ya wenzake katika majengo ya bunge Jumatano.

Kiranja wa wachache bungeni Junet Mohamed (kati) alipowaongoza wenzake 11 kukemea wandani wa Naibu Rais Dkt William Ruto kuhusu Gavana Joho Februari 06, 2019 katika majengo ya bunge. Picha/ Charles Wasonga

Aliandama na wabunge; Gladys Wanga (Mbunge Mwakilishi wa Homa Bay), Ken Chonga (Kilifi Kusini), Elisha Odhiambo (Gem), Omar Mwinyi (Changamwe), Mishi Mboko (Likoni) na Caleb Amisi (Saboti). Wengine walikuwa ni; Mark Nyamita (Uriri), Florence Mutua (Mbunge Mwakilishi wa Busia), Babu Owino (Embakasi Mashariki) na Godfrey Osostsi (Mbunge Maalum, ANC).

Wabunge hao walisisitisha kuwa gavana Joho ambaye ni naibu kiongozi wa chama cha ODM hajawahi kuhusishwa na biashara ya ulanguzi wa mihadarati, wakisema washukiwa wa uovu wamekamatwa au wanaandamwa.

“Tumechoshwa na madai kama hawa. Mbeleni tulisikia Gavana Joho hangesafiri ng’ambo kwa sababu alikuwa anasakwa. Ziara yake nchini Amerika 2018 ni ithibati kuwa madai hayana mashiko,” taarifa yao ikasema.

Mnamo Jumanne, Gavana Joho aliwashtaki Mbw Sang’ na wabunge; Oscar Sudi (Kapseret), Kimani Ichungwa (Kikuyu) na Didmus Barasa (Kimilili) kwa kumharibia jina.

Kwenye stakabadhi za kesi hiyo Bw Joho pia anadai kuwa madai ya wanasiasa hao wanne yatafanya wananchi wamchukie kwa kuhusishwa na biashara hiyo haramu.

Bw Joho anataka mahakama iwashurutishe Sang’ ana wenzake kumlipa fidia kwa kumharibia jina kupitia madai ya uwongo. Aidha, aliitaka mahakama kuwalazimisha wanne hao kumwomba msamaha kupitia taarifa katika magazeti yanayosomwa kwa wingi nchini.

Wiki iliyopita gavana huyo aliwapa wanasiasa hao makataa ya saa 24 wamwombe msamaha na kufuta kanda zote za video zenye matamshi hao katika mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, akihutubia wanahabari katika hoteli ya Serena Jumanne, Gavana Sang’ alisema kwamba kamwe hatamwomba msamaha Bw Joho. Badala yake, atawasilisha ushahidi kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuthibitisha madai yake.

“Sitamuomba msahama Bw Joho kwa sababu nina ushahidi tosha ambao nitawasilisha kwa DCI na EACC katika polisi wa kimataifa kuonyesha ukweli wa madai yangu,” akasema Bw Sang’ huku akipinga madai kuwa ametumwa na Dkt Ruto kuharibia Joho sifa.