Habari Mseto

Madaktari na wauguzi wakaa ngumu wagonjwa wakifa

August 19th, 2019 2 min read

FARHIYA HUSSEIN, WINNIE ATIENO na ANGELINE OCHIENG

WAHUDUMU wa afya na madaktari katika kaunti tofauti wameapa kuendeleza migomo yao hadi serikali za kaunti zitakapowalipa.

Wiki iliyopita, serikali kadhaa za kaunti ziliahidi kulipa wafanyakazi wao ifikapo Ijumaa iliyopita lakini imebainika kuna wahudumu wa afya ambao hawajapokea mishahara yao ya Julai.

Katika Kaunti ya Mombasa, wahudumu wa afya na madaktari walitoa wito kwa serikali ya kaunti kuwalipa mishahara yao wakisema wanataabika na kukosa pesa za kununua mahitaji yao muhimu na hata nauli ya kufika kazini.

Wakiandamana nje ya hospitali kuu ya Pwani, zaiid ya madaktari na wahudumu wa afya 300 walisema wagonwja wanateseka bila huduma ya afya.

“Serikali ya kaunti ina uwezo wa kutulipa mshahara wetu lakini hawataki. Hatuwezi kwenda kazini bila nauli ama hata pesa za kununua vyakula. Tuna mahitaji yetu kama binadamu yeyote yule. Huu ni unyama, ingekuwa serikali kuu inawacheleweshea mishahara yenu nina hakika magavana wangelikuwa wameenda mahakamani,” alisema Dkt Chibanzi Mwachonda.

Dkt Mwachonda ambaye ni naibu katibu mkuu wa chama cha madaktari nchini, alisema huduma za afya zimelemaa katika hospitali za umma huku wagonjwa wakitaabika.

Alimshtumu Gavana Hassan Joho kwa kuwacheleweshea wafanyikazi wa umma katika kaunti ya Mombasa mishahara yao akisema ni unyama.

“Anaweza kutulipa mishahara yetu kupitia mfuko wa kaunti wakisubiri fedha kutoka serikali kuu. Mombasa serikali ya kaunti ya Kwale imewalipa wafanyikazi wake? Kwani Mombasa ni spesheli?” aliuliza.

Madaktari hao ambao walisusia kazi tangu wiki iliyopita wanaitaka serikali kuu kuingilia kati maswala yao.

Wafanyakazi hao wa kaunti walisisitiza walipwe kabla mwezi huu kuisha.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo, ulibaini kuwa wagonjwa wengi waliachwa bila huduma huku wakilazimika kwenda hospitali za kibinafsi.

Katika Kaunti ya Kisumu, wahudumu wa afya waliendeleza mgomo wao kwa wiki ya pili baada ya serikali ya kaunti kushindwa kutekeleza ahadi ya kuwalipa Ijumaa iliyopita.

Waliapa kuzidisha mgomo wao ikiwa hawatalipwa mishahara yao ya Julai ifikapo Jumatano. Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi Kitaifa (KNUN) tawi la Kisumu, Bw Maurice Opetu alisema ni sharti serikali ya kaunti hiyo itambue hakuna maendeleo ya kiuchumi yanaweza kupatikana bila huduma bora za afya ya umma.