Habari

Madaktari wa Cuba waitwa Nairobi

April 15th, 2019 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

ATHARI za tukio la washukiwa wa Al-Shabaab kuwateka nyara madakari wawili wa Cuba waliokuwa wakihudumu kaunti ya Mandera Ijumaa iliyopita zimeanza kushuhudiwa baada ya serikali kuwaita ghafla jijini Nairobi madaktari wote wa Cuba wanaohudumu kwenye kaunti za mpakani mwa Kenya na Somalia.

Utafiti uliofanywa na Taifa Leo Dijitali Jumatatu ulibaini kuwa madaktari wawili wa Cuba waliokuwa wakihudumia hospitali za Lamu tayari walikuwa wamesafirishwa jijini Nairobi.

Kaunti zingine ambazo zilishuhudia kuhamishwa ghafla kwa madaktari wa Cuba ni Garissa na Wajir.

Akizungumza na wanahabari Jumatatu, Waziri wa Afya wa Kaunti ya Lamu, Dkt Anne Gathoni, alisema madaktari hao wawili walisafiri ghafla jinini Nairobi mwishoni mwa juma kwa kile alichokitaja kuwa ni kutafuta ushauri baada ya tukio la kutekwa nyara kwa wenzao wawili eneo la Mandera kuwaathiri kisaikolojia.

Bi Gathoni aidha hakueleza wazi iwapo madaktari hao wangerudi Lamu hivi karibuni.

Madaktari wawili wa Cuba wakitembezwa hospitalini King Fahad na Afisa Mkuu Msimamizi wa zamani wa hospitali hiyo, DFkt Ahmed Farid. Madaktari hao walikuwa wamewasili Lamu Julai 2018. Picha/ Kalume Kazungu

“Ni kweli. Madaktaari wetu wawili kutoka Cuba ambao wamekuwa wakihudumia hospitali zetu za Lamu walilazimika kusafiri ghafla jijini Nairobi. Bali na kuhofia usalama wao baada ya utekaji nyara wa wenzao kule Mandera, tukio hilo kwa jumla pia limewaathiri sana kisaikolojia.

“Wameenda nje ya Lamu kutafuta ushauri kwanza na sina ufahamu wowote kuhusu ni lini hasa watarudi hapa. Ni jambo ambalo tayari linajadiliwa,” akasema Bi Gathoni.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali  kwa njia ya simu, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Joseph Kanyiri pia alithibitisha kuondoka kwa madaktari hao wa Cuba Lamu lakini akapinga uhusiano wowote wa kuondoka kwao na kisa cha Mandera.

Alisema madaktari hao waliondoka baada ya kuitwa rasmi jijini Nairobi na serikali ili kujadili hali yao ya utendakazi ambalo ni jambo la kawaida.

“Ni kweli. Serikali imewaita madaktari wetu wa Cuba kutoka hapa Lamu jijini Nairobi. Ni mwito wa kawaida wala hauhusiani kivyovyote na tukio la kutekwa nyara kwa wenzao, Kaunti ya Mandera ambayo iko maili nyingi mbali na Lamu.

“Ikumbukwe kwamba tangu waletwe Lamu hawajakutana na mwaajiri wao Nairobi. Ni jambo la kawaida kwa maafisa wa umma, ikiwemo sisi kuitwa Nairobi ili kueleza hali ya utendakazi wetu kwa wakubwa wetu,” akasema Bw Kanyiri.

Madaktari wa Cuba wakimpongeza Waziri wa Afya, Sicily Kariuki alipowatembelea hospitalini King Fahad na kuzindua rasmi kitengo cha matibabu ya figo na kile cha wagonjwa wanaohitaji picha za tarakilishi (CT-SCAN) mnamo Novemba 16, 2018. Picha/ Kalume Kazungu

Wakazi tuliosema nao kisiwani Lamu baada ya kupokea habari za kuondoka ghafla kwa madaktari hao wa Cuba hospitalini walitaja hatua hiyo kuwa pigo kubwa kwa sekta ya afya eneo hilo.

Walisema ujio wa madaktari wa Cuba miezi kumi iliyopita ulikuwa umesaidia pakubwa kupunguza visa vya rufaa ya wagonjwa kutoka Lamu hadi kwenye maeneo ya Malindi, Kilifi, Mombasa na Nairobi kama ilivyokuwa ikishuhudiwa awali.

“Kusema kweli tunasikitika sana na kuondoshwa kwa madaktari wetu wa Cuba hapa Lamu. Wametusaidia pakubwa tangu walipofika hapa. Kesi za wagonjwa kupewa rufaa ya matibabu nje ya Lamu tayari zilikuwa zimepungua. Serikali iwarudishe madaktari hao,” akasema Bi Fatma Bule.

Bw Ahmed Khalifa aliitaka serikali kuimarisha zaidi usalama kwenye kaunti za Lamu, Mandera, Wajir na Garissa ili madaktari wawe na uhuru wa kufanya kazi kwenye mazingira salama.

Madaktari hao wa Cuba walianza kuhudumu Lamu baada ya kupelekwa huko na serikali kuu mnamo Julai, 2018.