Habari Mseto

Madaktari wa Hospitali ya Mama Lucy kizimbani kwa ulanguzi wa watoto

November 18th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

DAKTARI Mkuu katika Hospitali ya Mama Lucy iliyoko mtaa wa Umoja III Nairobi pamoja na msimamizi wa masuala ya hospitali hiyo walifikishwa kortini Jumatano kwa madai wanahusika katika mtandao wa ulanguzi wa watoto wachanga.

Polisi walifichua kuwa vinara hao wa hospitali Dkt Emma Mutio na Dkt Regina Musembi wanahusika na ulanguzi wa watoto wa kati ya umri wa siku moja hadi miezi minane.

Walipofikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bw Bernard Ochoi, wawili hao waliandamana na muhudumu wa masuala ya kijamii hospitalini humo Bw Makallah Fred Leparan.

Watatu hao watafunguliwa mashtaka ya ulanguzi wa watoto katika hospitali hiyo.

Kukamatwa kwa watatu hao kulifuatia ufichuzi kwenye taarifa iliyopeperushwa na shirika la kimataifa la habari BBC. Polisi waliwavamia watatu hao na kuwatia nguvuni.

Mbele ya Bw Ochoi, afisa mkuu katika masuala ya uchunguzi wa jinai Bw Wanga Masake alisema uchunguzi wa kina kuhusu kashfa hiyo ya kuuza watoto utafanywa kwa lengo la kuwashika wahusika wote.

“Tayari polisi wameweza kuwapata watoto wawili. Uchunguzi ni juu ya watoto wasiojua kuzugumza wanahitaji msaada wa mtu mzima,” alisema Bw Masake.

Afisa huyo aliomba polisi wapewe siku 10 kuwahoji watatu hao na kutembelea miji ya malezi ya watoto kukusanya taarifa za ujasusi kuhusu suala hilo.

Mahakama iliombwa isiwaachilie kwa dhamana kwa vile watavuruga ushahidi kutokana na ushawishi wao mkubwa. Insp Masake aliomba washukiwa hao wazuiliwe kwa muda wa siku 10 kuwezesha uchunguzi kukamilishwa.

Ombi la kuwazuilia siku 10 lilipingwa vikali na wakili Danstan Omari aliyesema madaktari hao wakuu walianza kufanya kazi hospitalini humo siku 10 zilizopita na kamwe hawakuhusika.

“Dkt Mutio alihamishwa kutoka hospitali ya Mbagathi siku 10 zilizopita naye Dkt Musembi alianza kufanya kazi hospitalini humo Juni 10 mwaka huu,” alisema Bw Omari

Bw Omari alifichua kuwa visa vya kuibwa kwa watoto viliripotiwa Mei mwaka huu na polisi hawakuchukua hatua hadi pale shirika la BBC lilipotangaza kashfa hiyo.

Wakili Danstan Omari (mwenye barakoa nyeupe) aliyewawakilisha Makallah Fred Leparen, Dkt Emma Mutio na Dkt Regina Musembi. PICHA/ RICHARD MUNGUTI

Mahakama ilifahamishwa na wakili Omari kuwa Dkt Mutio alihamishwa kutoka hospitali hiyo ya Mama Lucy siku 10 zilizopita baada ya ripoti kuenea kwamba watoto wanaibwa hospitalini humo.

Dkt Musembi, hakimu alifahamishwa, alianza kuhudumu katika hospitali hiyo Juni 2020. Bw Omari alisema Dkt Mutio alikuwa anasimamia hospitali ya Mbagathi wakati mapambano ugonjwa wa Covid-19 ulikuwa umechacha.

“Madaktari hawa wawili ni mashujaa wa kupambana na Covid-19. Hawapasi kuwa ndani ya seli za polisi ila wanatakiwa kuwa wakiendeleza ujuzi wao katika kuangamiza Corona,” alisema Bw Omari.

Dkt Mutio amehudumia Serikali tangu mwaka wa 2017 ilhali Dkt Musembi alianza kutoa huduma zake 1994.

Hakimu aliombwa awachilie watatu hao kwa dhamana na kuwaamuru wasithubutu kuvuruga uchunguzi. Polisi walidai endapo wawili hao wataachiliwa kwa dhamana wakati huu basi mashahidi watatishwa na wanaoficha watoto watahepa.

Lakini wakili alisema polisi wanajua makazi ya washukiwa hao katika mitaa ya KMA Langata, Greenspan na Umoja III.

Bw Ochoi aliamuru watatu hao wazuiliwe hadi Alhamisi atakapoamua ikiwa atawaachilia kwa dhamana ama ataamuru wazuiliwe kwa siku kumi polisi wawahoji na kukamilisha uchunguzi.

Hakimu aliamuru polisi waendelee na uchunguzi huku akiandaa uamuzi wake.