Habari Mseto

Madaraka Dei: Mshukiwa wa ugaidi akamatwa akijaribu kuingia Narok Stadium

June 1st, 2019 1 min read

Na NYABOGA KIAGE na SAMMY WAWERU

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 22 Jumamosi asubuhi alitiwa nguvuni akijaribu kuingia kinyume cha sheria katika uwanja wa Narok, ambapo sherehe za maadhimisho ya Madaraka Dei 2019 zimefanyika.

Rais Uhuru Kenyatta ndiye ameongoza taifa kuadhimisha sherehe hizo ambazo ni makala ya 56.

Awali iliripotiwa kuwa Adan Galhai ambaye pia anajulikana kama Urisha Galhai alikuwa amekamatwa na maafisa wa KDF lakini akaponyoka.

Kwa mujibu wa maelezo ya ripoti ya idara ya polisi, imebainika kuwa Galhai anayeshukiwa kuhusishwa na kundi haramu la Al Shabaab, alijifanya kuwa afisa wa usalama.

“Rais Uhuru Kenyatta akikagua gwaride la heshima katika uga wa Narok Juni 1, 2019, mshukiwa alitaka kuingia uwanjani. Ijumaa alishikwa na maafisa wa KDF, na alipopekuliwa kitambulisho chake cha kitaifa na ‘kitambulisho’ kuwa ni afisa wa usalama, vilipatikana. Alihepa alipotakiwa kujibu maswali,” inaeleza ripoti ya polisi.

Taifa Leo imearifiwa kuwa mshukiwa alirejea tena mapema Jumamosi, na hapo ndipo alikamatwa.

Mwanamume mwingine aliyeandamana naye alifanikiwa kutoroka.

Maafisa wa polisi wanaofuatilia suala la mshukiwa walifichua kwamba alidanganya alikesha kwenye hoteli moja karibu na uwanja wa Narok.

Kulingana na idara ya polisi, Galhai alibadilisha dini mwaka 2014 na kuwa Mwislamu.

Inadaiwa amekuwa akiishi mtaani Eastleigh, jijini Nairobi.

Usalama katika uwanja wa Narok ulikuwa umeimarishwa ndani na nje, wakati maadhimisho ya Madaraka Dei yakiendelea.