Habari

Madaraka Dei: Tusiogope kubadilisha Katiba – Uhuru

June 1st, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Madaraka Dei ya mwaka huu, shughuli zinazoshirikishwa katika hafla hiyo ya kitaifa zimeendeshwa kwa njia ya runinga, redio na mtandao kwa mbashara kutoka Ikulu ya Nairobi.

Hafla hiyo imehudhuriwa na watu wachache Jumatatu, wengi wao wakiwa viongozi wakuu serikalini na wanasiasa, kutokana na kanuni za kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid – 19 nchini.

Rais Uhuru Kenyatta ameongoza taifa katika maadhimisho. “Tusiogope kubadilisha vipengele mbalimbali vya katiba, ikiwa mabadiliko hayo yatafaa taifa kwa sasa na siku za usoni,” Rais akasema akiashiria kuwepo kwa mabadiliko ya Katiba, yanayoleta uongozi jumuishi serikalini.

Kauli ya Rais Kenyatta imelenga ripoti ya tume ya maridhiano, BBI, iliyotolewa baada ya salamu za heri njema kati yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga, maarufu kama Handisheki, hapo Machi 2018.

Kama ilivyo desturi na tamaduni, Rais Kenyatta pia amekagua gwaride la heshima lililoandaliwa na kikosi cha wanajeshi wa Kenya, KDF.

Maadhimisho haya yamejiri wakati ambapo Wakenya wanalia kuhangaishwa na athari za corona, janga ambalo ni la kimataifa.

Kafyu ya kitaifa na amri ya kutotoka na kuingia katika baadhi ya kaunti, ili kuzuia msambao wa Covid – 19, imechangia katika kudorora kwa uchumi, wananchi wakiwa na matumaini baada ya Juni 6, Rais ataondoa amri hiyo.

Kwa kawaida, hafla hii huandaliwa katika uga mbalimbali nchini kila mwaka na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu.

Wahubiri wa madhehebu, hupewa fursa kukabidhi taifa kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya maombi, ikiwa ni pamoja na kushukuru.

Aidha, ni wahubiri watatu pekee walioongoza taifa katika sala. “Wakati huu tunaadhimisha Madaraka Dei 2020, tunamuomba Mwenyezi Mungu atukumbuke na kutuondolea janga hili la Covid – 19,” akasema Askofu Jackson Ole Sapit wa Kanisa la Kianglikana, ACK.

Kwa njia ya sala zilizorekodiwa, kutoka kanisa la ACK, Nairobi, Askofu Ole Sapit pia alikumbuka waathiriwa wa janga la mafuriko, ambalo kufikia wiki iliyopita lilikuwa limesababisha maafa ya watu 285.

Kinyume na hafla zingine, ambapo tamasha za nyimbo hutumbuizwa moja kwa moja uwanjani, hafla ya leo zilikuwa zimerekodiwa.

Rais Uhuru Kenyatta ameongoza taifa katika kuadhimisha Madaraka Dei mwaka huu. Viongozi wengine wakuu serikalini waliohudhuria hafla hiyo iliyopeperushwa kutoka Ikulu kwa njia ya runinga ni pamoja na Naibu wa Rais Dkt William Ruto, Jaji Mkuu (CJ) David Maraga, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya, Maspika wa mabunge yote mawili, miongoni mwa wengine.

Gavana wa Nairobi Mike Sonko na kiongozi wa ODM Raila Odinga pia wamehudhuria.

Wakati huo huo, Rais Kenyatta amebuni mpango wa kutambua Wakenya wazalendo waliojitolea kwa hali na mali kuangazia athari za janga la Covid – 19.

Mpango huo ‘Uzalendo Award’, kulingana na Rais Kenyatta unalenga kuwatuza waliojituma kutoa huduma za kimsingi, kuonyesha uzalendo, na kusaidia katika oparesheni kuangazia athari za virusi vya corona.

Miongoni mwa waliotuzwa na mwandishi maarufu wa habari na makala ya afya katika gazeti la ‘Daily Nation’, Bi Nasibo Kabale.

Rais alitoa tangazo hilo mnamo Jumatatu alipoliongoza taifa katika maadhimisho ya Madaraka Dei 2020, makala ya 57, katika hafla iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia runinga kutoka Ikulu, Nairobi.

Alisema tayari majina ya watakaotambuliwa yamechapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali. “Wanahitaji kutambuliwa katika jitihada zao kusaidia kuangazia Covid – 19,” Rais Kenyatta akaeleza, kwenye hotuba yake kwa taifa.

Uzalendo Award, inawiana na tuzo zinazotolewa kila mwaka na kiongozi wa taifa ndizo HSC Award, zinazotambua waliofanya makuu katika jamii.

Rais alisema serikali yake itaendelea kuimarisha mikakati kuangazia janga la Corona, ambalo sasa ni kero la kimataifa. “Kama serikali inayojali maslahi ya raia wake, tunaendelea kuimarisha mikakati kuokoa maisha ya Wakenya. Ili kupunguza bei ya bidhaa, tumepunguza ushuru, VAT, kutoka asilimia 16 hadi 14,” akasema.

Covid – 19 imeathiri uchumi wa taifa na sekta mbalimbali. Athari zimekuwa wengi kupoteza nafasi za ajira, biashara kufungwa na maelfu kushindwa kukidhi mahitaji ya kimsingi.