Habari Mseto

Madeni sasa yamelemea nchi – Sapit

October 14th, 2019 2 min read

Na GEORGE ODIWUOR

KANISA la Anglikana (ACK) na Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu na Uwekezaji (PAIC) wameelezea hofu yao kuhusu ongezeko la madeni ambayo sasa yamefika zaidi ya Sh5.8 trilioni.

Kiongozi wa kanisa la ACK nchini Jackson Ole Sapit na mwenyekiti wa PAIC Moses Kajwang walisema kuwa nchi imelemewa na mzigo mzito wa madeni ambayo yameathiri uchumi wa nchi.

Askofu Mkuu Sapit alisema huenda serikali ikalazimika kuongeza ushuru bidhaa muhimu ili kupata fedha za kulipa madeni. Bw Kajwang ambaye ni Seneta wa Homa Bay alisema kuwa mswada uliopitishwa na Bunge la Kitaifa ili kuruhusu serikali kukopa kiasi kinachofikia Sh9 trilioni unafaa kupelekwa katika Seneti ili ujadiliwe na maseneta.

Bw Kajwang alisema kuwa uchumi wa nchi hii huenda ukazorota iwapo serikali itaruhusiwa kukopa Sh3.2 trilioni zaidi. Alisema Bunge la Kitaifa halifai kuachiwa jukumu la kujadili mswada huo bila kushirikisha Seneti.

“Ikiwa bunge la Seneti litakosa kuafikiana na Bunge la Kitaifa, basi suala hilo linastahili kupelekwa kortini ili kupata mwelekeo,” akasema Kajwang.

Askofu Mkuu Sapit alisema Kanisa la ACK limeingiwa na wasiwasi kutokana na kuongezeka kwa madeni hasa ya nchi za kigeni. Alisema fedha zinazokopwa zinafaa kusaidia Wakenya maskini kujiinua kiuchumi badala ya kuishia mifukoni mwa wachache huku walipa-ushuru wakiumia.

“Mikopo tunayochukua kutoka nchi za kigeni inafaa kuboresha maisha ya wananchi,” akasema Bw Sapit.

Kustaafu

Wawili hao walikuwa wakizungumza mjini Homa Bay katika hafla ya kumuaga aliyekuwa kiongozi wa ACK eneo la Nyanza Kusini, Askofu James Ochiel ambaye amestaafu.

Kiongozi huyo wa ACK alishutumu baadhi ya viongozi serikalini ambao wamekuwa wakijitajirisha wenyewe huku mamilioni ya Wakenya wakihangaika.

Alipongeza Kanisa Katoliki kwa kuweka masharti makali ili kuzuia fedha za ufisadi kuingia kanisani.

Alisema Kanisa la ACK litakubali fedha zinazoletwa kanisani na wanasiasa tu ikiwa fedha hizo ni ‘safi’.

Seneta wa Homa Bay alisema kuwa serikali haifai kukopa hela zaidi ili kufadhili miradi ambayo imesambaratika kama vile mradi wa kilimo wa Galana Kulalu.