Habari Mseto

Madeni tele KMC huku serikali ikikiri kulemewa na kazi

April 3rd, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

KIWANDA cha Nyama nchini, Kenya Meat Commission (KMC) kinazidi kuzongwa na madeni ya mamilioni ya pesa za wakulima wa mifugo, huku juhudi za kukibinafsisha zikiendelea.

Wakuu wa kiwanda hicho jana walikiri mbele ya Kamati ya Bunge la Seneti Kuhusu Kilimo kuwa wakulima wanakidai zaidi ya Sh250 milioni, huku wafanyakazi wake pia wakikidai Sh144 milioni.

Meneja Msimamizi wa KMC James Ole Seriani alikiri kuwa jumla ya Sh89 milioni ni deni la wakulima ambao mifugo wao walinunuliwa wakati wa kiangazi kuwaokoa kutokana na hasara, huku zingine zikiwa za wakulima ambao wameuzia kiwanda hicho mifugo lakini wakakosa kulipwa.

Waziri Msaidizi wa Kilimo Andrew Tuimur aidha alikiri kuwa serikali imeshindwa kusimamia KMC, akisema hata sasa kinahitaji kushikiliwa, kabla ya mpango wa kukibinafsisha kukamilika.

“Uwezo wake wa kazi umekuwa ukididimia na idadi ya mifugo ambao kinachinja kwa siku kupungua kwani hata baadhi ya mashini zinazotumika zilinunuliwa kama miaka 60 iliyopita. Suluhu ya pekee ni kwa KMC kubinafsishwa kwani serikali imeshindwa kukisimamia,” akasema Bw Tuimur.

Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Kajiado Mary Seneta alilalamika kuwa maelfu ya wakulima wanahangaika kwani hawajalipwa na kiwanda hicho, akilaumu wizara hiyo kwa kuegemea aina zingine za kilimo na kutelekeza wafugaji.

Aidha, katika suala la ubinafsishaji wa mashirika ya serikali, wizara hiyo ilikataa kutoa habari mbele ya kamati hiyo kuhusu namna imepanga kubinafsisha viwanda vya sukari, ikisema kazi hiyo inaendeshwa na Tume ya Ubinafsishaji.

Seneta wa Migori Ochilo Ayacko, hata hivyo, aliitaka wizara kuunda timu ya kuhakikisha kuwa mali ya viwanda hivyo inalindwa wakati huu, akisema kuwa tayari baadhi ya watu wameanza kupora kiwanda cha Sony baada ya habari za kuwa kitabinafsishwa kuibuka.

“Kunahitajika watu wa kuchunga ama hakutakuwa na kitu cha kubinafsishwa wakati wa mwisho. Tayari baadhi ya watu wanapora,” akasema Bw Ayacko.

Wizara hiyo aidha imeahidi kutumia Sh800 milioni ambazo iliomba wizara ya Fedha kwenye bajeti ya ziada kuwalipa wakulima wa kiwanda cha Chemelil madeni yao, kwani hawakulipwa wakati wakulima wa viwanda vingine walipolipwa.