Habari Mseto

MADENI: Uchumi wa Kenya katika hatari ya kuzama

May 10th, 2020 2 min read

Na DAVID MWERE

MIKOPO tele iliyochukuliwa na serikali kwa miaka michache iliyopita, sasa inaweka Kenya katika hatari kubwa ya kuzama kiuchumi.

Wakati huu wa janga la corona, Kenya ni miongoni mwa mataifa yanayoathirika sana kiuchumi.

Kwa msingi huu, wataalamu wanasema ingehitajika taifa litenge fedha ambazo zingesaidia kufufua uchumi wakati janga la corona litakapoondoka. Badala yake, imebainika fedha nyingi zimetengewa ulipaji madeni kwenye bajeti ya mwaka huu wa kifedha.

Wataalamu hao sasa wanapendekeza serikali iangalie upya makadirio ya bajeti hiyo ya Sh3.15 trilioni ya mwaka wa kifedha wa 2020/2021.

Afisi ya Bajeti katika Bunge (PBO) pamoja na Mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria, walitambua kwamba katika bajeti hiyo ambayo ndiyo kubwa zaidi kuwahi kuwepo nchini, fedha zilizotengewa masuala ya corona ni Sh2.6 bilioni pekee.

Hizi si fedha ambazo zitatumiwa kuinua uchumi na kulinda wananchi kiriziki, bali zimenuiwa kutumiwa kupima wananchi kwa wingi ili kubainisha walioambukizwa virusi vya corona.

“Kwa kuzingatia janga linalotukumba, mkakati mwafaka ambao umeshuhudiwa kimataifa, ungekuwa ni kutenga fedha za kufufua uchumi. Hili lisiwe tu kwa minajili ya kusaidia kiafya na kimapato katika kipindi hiki cha sasa, bali kwa ufadhili wa awamu nyinginezo za kuboresha uchumi baada ya janga la corona. Bajeti ya 2020/2021 imefeli katika hili,” afisi hiyo ikaonya, kupitia kwa arafa iliyowasilishwa bungeni.

Madeni

Madeni ya Kenya kwa jumla yalipita Sh6 trilioni kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2019, kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Kenya (CBK).

Baadhi ya mikopo ilichukuliwa kutoka China na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta, ikisemekana itatumiwa kustawisha miundomsingi.

Hata hivyo, wachanganuzi wa kiuchumi na baadhi ya wanasiasa hukashifu serikali kwa kutumia vibaya fedha hizo kwani mwananchi wa kawaida hajanufaika.

Inahofiwa China inaweza kutwaa mali muhimu za taifa ikiwa Kenya itashindwa kulipa madeni hayo kwa muda unaofaa, kama vile Bandari ya Mombasa, ingawa serikali hukana kulikuwa na makubaliano ya aina hii.

Mataifa ya Afrika yamekuwa yanajikakamua kuomba nchi za nje ziwaruhusu kutolipa madeni hadi janga la corona litakapoondoka, lakini suala hili halijafaulu kufikia sasa.

“Endapo China itakubali kupunguza mzigo wa madeni, itasaidia kuondoa dhana kwamba walituwekea mtego,” mtaalamu wa masuala ya kifedha kimataifa, Bw Leonard Wanyama, akasema.

Kwa sasa, serikali inahitaji kukopa Sh1.3 trilioni nyingine kujaza pengo katika makadirio ya bajeti. Hii itaongeza madeni hadi takriban Sh7.2 trilioni.

“Hili haliwezi kugharamiwa. Omba omba hawana aibu. Inafaa tuambie wale tuliokopa kutoka kwao kwamba hatuna uwezo wa kugharimia madeni yetu hadi mwaka wa 2023. Hivyo, tutapata Sh1 trilioni ya ziada kila mwaka kwa miaka mitatu,” akasema Mbunge Kuria, ambaye pia ni mtaalamu wa kifedha.

Hayo yanatokea wakati ambapo karibu shughuli zote muhimu za kiuchumi zimekwama, na zile chache zinazoendelea zikiwa zinajikokota.

Bw Kuria, kwenye taarifa yake, alisema Kenya ilikuwa tayari inatatizika sana kifedha kabla ya janga la corona, na hali itakuwa mbaya zaidi kama maafisa serikalini hawatatumia busara kuhusu bajeti ya taifa na matumizi