Dondoo

Madeni ya vipodozi yamaliza ndoa yake

February 22nd, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

SHANZU, MOMBASA

Kioja kilizuka eneo hili baada ya polo kumtimua mkewe alipogundua kwamba alikuwa na madeni mengi ya vipodozi.

Kulingana na mdokezi, wawili hao walikuwa wamemaliza miezi miwili katika ndoa.

Walipokuwa wakichumbiana, polo alikuwa akishangazwa na vipodozi na mavazi ya bei ghali aliyokuwa akivalia mrembo.

Polo alianza kushuku mwanadada alikuwa na sponsa wa nguvu sana. Yasemekana mambo yalimuendea kombo kipusa baada ya wenye madeni kuanza kumdai.

Penyenye zinasema demu alikuwa amewakopa pesa karibu marafiki wake wote alizokuwa akitumia kununua vipodozi na mavazi.

Baadhi ya waliomdai walienda hadi kwa mumewe kumdai. Inadaiwa kipusa alikuwa amewaelekeza baadhi yao kwake huku akifikiri polo angemlipia madeni hayo.

Kulingana mdokezi, kipusa aliamua kumueleza polo kuhusu yaliyokuwa yakiendelea.

Baada ya kusikia kiwango cha hela alichokuwa akidaiwa, polo alimuamrisha ashike njia na kurudi kwao.

“Kazi yako ilikuwa ni kukopa pesa kutoka kwa kila mtu! Hauna aibu kuniambia. Nijiuze ndio nipate hizo pesa!” polo alimshtumu kipusa.

Polo aliamua kumtimua kipusa huku akiwaeleza waliomdai wajipange. “Mimi sikuoa madeni. Mtajipanga na yeye. Na tena simtaki kwangu. Huyu ataniletea hasara,” polo alidai.

Kipusa alimuomba polo msamaha lakini wapi. “Nimesema rudi kwenu. Wewe utanipora. Hata pengine umeshaenda benki na kuchukua mkopo kwa jina langu. Kwenda kabisa,” polo alimtimua kipusa.

Wenye madeni walikuwa pale wakitazama akitimuliwa na mumewe.