Madeni yaanza kuuma

Madeni yaanza kuuma

Na WANDERI KAMAU

WAKENYA wameanza kuhisi makali yanayotokana na masharti yaliyowekwa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia (WB) kwa Kenya baada ya kuipa nchi hii mikopo hivi majuzi.

Mnamo Februari, Kenya ilifanikiwa kupata mkopo wa Sh256.3 bilioni kutoka kwa IMF, ambao utatolewa kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuisaidia serikali kukabili makali ya virusi vya corona na kustawisha uchumi.

Mikopo hiyo inaandamana na masharti makali ambayo mashirika hayo yanasema ni ya kusaidia kupunguza wizi, matumizi mabaya ya fedha za umma na kulainisha usimamizi wa uchumi.

Ili kutekeleza masharti hayo, maelfu ya watumishi wa umma wanatarajiwa kupoteza ajira kutokana na marekebisho ambayo IMF na WB zinataka serikali ifanyie taasisi za umma.

Wiki iliyopita, Waziri wa Fedha, Ukur Yatani aliunganisha Idara ya Kustawisha Biashara na Viwanda (ICDC), Benki ya Kustawisha Biashara (IDB) na Idara ya Kustawmi.

Ili kutekeleza masharti hayo, maelfu ya watumishi wa umma wanatarajiwa kupoteza ajira kutokana na marekebisho ambayo IMF na WB zinataka serikali ifanyie taasisi za umma.

Wiki iliyopita, Waziri wa Fedha, Ukur Yatani aliunganisha Idara ya Kustawisha Biashara na Viwanda (ICDC), Benki ya Kustawisha Biashara (IDB) na Idara ya Kustawisha Utalii (TFC) kubuni Halmashauri ya Kusimamia Maendeleo Kenya (KDC).

Serikali pia imependekeza kufutiliwa mbali kwa Mamlaka ya Kusimamia Biashara ya Hisa (CMA), Mamlaka ya Kusimamia Malipo ya Uzeeni (RBA), Mamlaka ya Kusimamia Bima (IRA) na Mamlaka ya Kusimamia Vyama vya Ushirika (SASSRA) na badala yake kuwa na halmashauri moja itakayosimamia na kulainisha masuala ya fedha nchini.

Mashirika mengine yanayotarajiwa kuunganishwa ni Mamlaka ya Kusimamia Uuzaji wa Biashara Nje ya Nchi (KEPA), Mamlaka ya Kusimamia Uwekezaji Kenya (KIA), Bodi ya Kusimamia Utalii (TB), Sekrerariati ya Kusimamia Utekelezaji wa Ruwaza 2030, Huduma ya Kuchunguza Ubora wa Mimea (KEPHIS) na Mamlaka ya Kitaifa Kusimamia Masuala ya Usalama wa Binadamu na Mimea (NBA).

Ikiwa waziri atakubali mapendekezo yaliyowasilishwa kwake, idara zaidi zitakazounganishwa ni Tume ya Kusimamia Filamu (KFC), Bodi ya Kusimamia Filamu Kenya (KFCB), Idara ya Kusimamia Hakimiliki za Bidhaa (IPI) na Mamlaka ya Kukabiliana na Bidhaa Ghushi (ACA).

Kwenye mapendekezo hayo, majukumu ya Bodi ya Uhariri wa Historia na Kumbukumbu Nchini (KYEB) yatahamishiwa kwa Makavazi ya Kitaifa.

Hatua hiyo za kuunganisha mashirika ya umma itayatapunguza kutoka 241 hadi 187, hatua ambayo itapelekea kupungua kwa idadi ya wafanyikazi baada ya kushikanishwa kwa majukumu.

Hayo yanajiri wakati serikali imeongeza kiwango cha ushuru unaotozwa bidhaa muhimu hasa gesi ya kupikia, kama masharti ya mikopo ya mashirika hayo mawili.

Mbali na kuunganishwa kwa mashirika, taasisi nyingine 14 zikiwemo Kenya Power (KP), Shirika la Reli Kenya (KR), Shirika la Habari (KBC), East African Portlands Company (EAPC), Shirika la Posta Kenya (PCK), vyuo vikuu vya Nairobi (UoN), Moi, Kenyatta zitafanyiwa marekebisho.

Tayari, Chuo Kikuu cha Nairobi kimetangaza kufutilia mbali baadhi ya nyadhifa, kuunganisha nyingine na kubuni mpya kwenye juhudi za kupunguza gharama ya kuendesha chuo hicho.

Pia kimeongeza karo maradufu, hatua ambayo huenda ikalemea wanafunzi kutoka familia maskini.

Kulingana na wadadisi wa masuala ya uchumi, ni lazima Wakenya wajitayarishe kwa kipindi kigumu zaidi kwani lazima serikali ifanye kila iwezalo kupata ushuru wa kufadhili miradi ya maendeleo na kulipa mikopo inayodaiwa na nchi za nje.

“Huu ni mwanzo tu. Tunaelekea katika wakati mgumu kiuchumi. Chini ya IMF, serikali haina uamuzi mwingine ila kufuata maagizo inayopewa,” asema mwanauchumi Tony Wetima.

Anasema Kenya inaelekea katika miaka ya tisini, ambapo serikali lilazimika kutekeleza masharti makali.

Hapo Jumanne iliibuka kuwa ada za maji zitaongezeka baada ya Benki ya Dunia kusema kuwa kampuni zinazotoa huduma za maji zinapaswa kufadhili bajeti ya Mamlaka ya Kudhibiti Huduma za Maji Kenya (WRA) kutoka asilimia 30 hadi 70.

“Ni wazi wananchi wanaumia kutokana na sera hizi. Hali inaendelea kudorora kwani deni la taifa linazidi kuongezeka,” asema Bi Wanjiru Gikonyo kutoka Taasisi ya Uwajibikaji wa Kijamii (TISA).

Hata hivyo, mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti, Kanini Keega, anasema ni kawaida serikali kukopa inapotekeleza miradi ya maendeleo: “Hatupaswi kuwa na hofu kwani hata nchi zilizostawi kiuchumi kama Amerika na Uingereza zina mikopo pia.”

You can share this post!

Ogier arudisha mkono kwa kumwaga Sh2.4 milioni kusaidia...

LSK yataka afisa apewe dhamana kabla ya kunaswa