Michezo

Madereva 25 tayari kuonyeshana ubabe KCB Nanyuki Rally

August 29th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MADEREVA 25 wako tayari kuonyeshana ubabe wao wa kuendesha magari katika duru ya tano ya Mbio za Magari za Kitaifa za Kenya (KNRC) ya KCB Nanyuki Rally itakayofanyika Agosti 31.

Bingwa mtetezi Carl ‘Flash’ Tundo pamoja na jagina Ian Duncan na Erick Bengi wanarejea mashindanoni baada ya kukosa raundi ya nne ya KCB Kilifi Rally wiki chache zilizopita, ambayo bingwa wa Afrika mwaka 2017, 2018 na 2019 Manvir Baryan alishinda.

“Mimi napenda sana duru ya Nanyuki kuliko zile zingine zote. Sikushiriki duru ya Kilifi kwa sababu ilikaribiana sana na duru ya Nanyuki…Bado nawinda taji la msimu huu, ingawa kukosa duru ya Kilifi imefanya kampeni yangu kuwa ngumu sana,” alisema Tundo.

Baldev Chager, ambaye anaongoza jedwali la mwaka huu kwa alama 102, amejiandikisha kuwania alama zaidi. Baryan pia yuko ulingoni sawa na mshindi wa KCB Nakuru Rally Onkar Rai, ambaye hajakuwa na bahati katika duru mbili zilizopita.

Tundo alishinda Nanyuki Rally mwaka 2018 akifuatwa na Baryan na bingwa wa KCB Kajiado na Safari Rally Chager katika usanjari huo.

Tundo alikuwa na msimu mzuri 2018 aliponyakua pia mataji ya Guru Nanak, Eldoret, Athi River, Safari Rally na KMSC Rally. Hata hivyo, atakuwa akitafuta ushindi wake wa kwanza msimu huu mjini Nanyuki.

Duncan, Onkar na Bengi ni baadhi ya madereva 11 waliojiuzulu katika makala yaliyopita ya Nanyuki Rally na watatumai nuksi hazitawaandama tena.

Msimamo wa alama baada ya duru ya nne (10-bora):

Baldev Chager (alama 102)

Manvir Baryan (73)

Carl Tundo (71)

Tejveer Rai (51)

Izhar Mirza (33)

Onkar Rai (25)

Sohanjeet Puee (25)

Ammar Haq (24)

Ian Duncan (23)

Jasmeet Chana (19)