Habari

Madereva wa matrela wageuka wasambazaji wakuu wa corona

May 12th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

MADEREVA tisa wa matrela Jumatatu walithibitishwa kuwa miongoni mwa watu 28 walioambukizwa virusi vya corona nchini, huku chama kinachowatetea kikilalama dhidi ya gharama ya juu ya wao kupimwa virusi hivyo.

Hali hiyo sasa imefikisha idadi ya watu walioambukizwa kuwa 700 tangu kisa cha kwanza kuthibitishwa nchini mnamo Machi.

Kulingana na Wizara ya Afya, madereva hao, ambao wote ni Wakenya, walithibitishwa kuambukizwa baada ya kukaguliwa katika eneo la Namanga, Kaunti ya Kajiado, kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania.

Kwenye kikao cha kila siku kuhusu hali ya virusi nchini, Naibu Waziri wa Afya, Rashid Aman alisema hilo linaashiria jinsi virusi hivyo vilivyo tishio kubwa kwa madereva hao.

Serikali pia ilisema iliwazuia madereva watano wa Tanzania kuingia nchini kupitia kituo hicho hicho, baada ya kuthibitishwa kuwa navyo.

Hilo linajiri huku serikali ikisisitiza kuwa, lazima madereva wa matrela zaidi ya 15,000 kote nchini wakaguliwe dhidi ya virusi hivyo kabla ya kuanza safari za kusafirisha mizigo kutoka bandari ya Mombasa.

Serikali pia imeweka vituo kadhaa barabarani ambapo madereva watahitajika kuonyesha vyeti kuhusu hali zao za afya.

Hilo pia linajumuisha hospitali maalum ambazo serikali imesisitiza ndizo pekee ambapo watakaguliwa ikiwa wameambukizwa au la.

Lakini Jumatatu, Chama cha Madereva wa Matrela (KTA) kilikosoa vikali kanuni hizo, kikizitaja kuwa uonevu.

Afisa Mkuu Mtendaji wa chama hicho, Bw Dennis Ombok alitaja hitaji la madereva kulipa ada ya Sh6,000 ili kukaguliwa kama dhuluma ya wazi dhidi yao.

Kanuni hizo zilitolewa na wizara hiyo Jumapili, kwenye juhudi za kudhibiti maambukizi ya virusi katika eneo la Afrika Mashariki.

“Lazima wizara itathmini upya kanuni hizo,” akasema.

Na kwenye takwimu zilizotolewa Jumatatu, idadi ya waliofariki ilifika watu 33 baada ya mtu mmoja zaidi kufariki.

Hata hivyo, idadi ya waliopona ilifikia watu 251 baada ya watu 12 kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Wale waliothibitishwa kuambukizwa Jumatatu wanatoka katika kaunti za Nairobi (7) Mombasa (10), Kajiado (9) na Wajir (2).

Serikali pia ilizindua nambari maalum ya WhatsApp, ambapo Wakenya watakuwa wakiitumia kupata maelezo yoyote kuhusu virusi hivyo. Nambari hiyo ni: 0110719719