Madereva wa tuktuk Githurai waonyesha umoja kuboresha kazi kwa kuchagua mwakilishi wao

Madereva wa tuktuk Githurai waonyesha umoja kuboresha kazi kwa kuchagua mwakilishi wao

Na SAMMY WAWERU

MADEREVA wa muungano wa wahudumu wa tuktuk na magari madogo aina ya maruti eneo la Githurai 45 (GTMA) wamefanya uchaguzi wa viongozi watakaokuwa wakiwawakilishi katika kuangazia matakwa yao.

Uchaguzi huo umejiri wiki moja baada ya wamiliki wa magari hayo ya usafiri na uchukuzi kuchagua viongozi wao.

Katika kinyang’anyiro cha madereva na kilichovutia wagombea saba, wawakilishi wawili pekee ndio walichaguliwa.

Bw Douglas Kimani maarufu kama Kim, aliibuka kidedea baada ya kuzoa kura 36, akifuatwa na mshindani wake wa karibu, Bw David Mongare aliyepata 34.

Uchaguzi huo ulishirikisha madereva 86 na wamiliki 51, idadi jumla ya waliopiga kura ikiwa 137.

Kura 3 pekee ndizo zilifutiliwa mbali, kwa sababu ya kutofuata sheria za uchaguzi.

Eneo la Githurai linakadiriwa kuwa na zaidi ya tuktuk na maruti 300, magari hayo yakijumuishwa.

“Ninaridhia imani ambayo madereva na wamiliki mmenipa kuongoza wafanyakazi wa GTMA. Tutashirikiana kwa karibu na wadauhusika wote kuimarisha kazi,” Bw Kimani akasema.

Bw David Mongare, na ambaye alikuwa wa pili katika zoezi hilo la kidemokrasia aliteuliwa kama msaidizi wa Kimani.

Uchaguzi wa kihistoria kuchagua mwakilishi wa madereva

Tangu huduma za uchukuzi kwa njia ya tuktuk zizinduliwe Githurai 2014, madereva hawajawahi kuwa na mwakilishi wao, uchaguzi huo ukitajwa kama wa kihistoria na uliosifiwa huenda ukasaidia kuimarika kwa utendakazi.

“Huu ni mwamko mpya. Huduma za tuktuk na maruti, ni miongoni mwa sekta za uchukuzi zinazoingiza mamilioni ya pesa. Si haki dereva kufanya kazi zaidi ya miaka mitatu, anaishia kukosa kuwa mmiliki wa gari.

“Chaguzi ndizo huamua uongozi bora na mbaya. Mkichagua mwenye maono, kazi itaboreka, kiongozi asiyejali kazi itafilisika. Malengo yetu kama viongozi tuliochaguliwa, mbali na kujali maslahi ya wamiliki tunataka kuweka mikakati maalum madereva waliohudumu muda mrefu nao pia wawe wamiliki, kwa kuwasaidia kununua tuktuk,” akasema Bw Laban Gitonga, mwenyekiti wa wamiliki katika GTMA.

Aliambia Taifa Leo kwenye mahojiano kwamba afisi iliyoko inalenga kuweka mikakati ya uwekaji akiba, hatua itakayosaidia kuimarisha maslahi ya wamiliki na pia madereva.

Huduma za tuktuk na maruti katika eneo la Githurai zimeonekana kuvutia serikali ya kitaifa na ya Kaunti ya Kiambu, kutokana na ukusanyaji wa kodi na ushuru.

Ni kati ya sekta zinazosaidia kuimarisha uchumi katika eneobunge la Ruiru.

Mbunge wa eneo hilo, Bw Simon King’ara ameahidi wahudumu hao kuwa atawapiga jeki kwa kima cha Sh50, 000 kuanzisha mradi wa uwekaji akiba.

Madereva wa tuktuk Githurai waonyesha umoja kuboresha kazi kwa kuchagua mwakilishi wao. Mwakilishi wa madereva wa muungano wa tuktuk na maruti Githurai (GTMA), Bw Douglas Kimani (kushoto) aliyechaguliwa. Atakuwa akisaidiwa na Bw David Mongare (aliye katikati). Picha/ Sammy Waweru

Wakati wa uchaguzi wa viongozi wa wamiliki, Bw King’ara alihimiza GTMA kuanzisha kundi au Chama cha Ushirika (Sacco) ili kunufaika na mikopo ya serikali.

Muungano huo hata hivyo umesajiliwa chini ya Idara ya Masuala ya Jinsia Utamaduni na Huduma za Kijamii (SCDO).

Uchaguzi wa madereva ulianza mwendo wa saa nne asubuhi na kukamilika saa tisa alasiri, ambapo kila mpiga kura aliyejitokeza majina yake yalikaguliwa kwenye sajili ya madereva na wamiliki ili kuepuka udanganyifu na wizi wa kura.

Baada ya kuchagua, mpiga kura alipakwa rangi kwenye kidole ili kuzuia upigaji kura mara ya pili.

Shughuli hiyo iliendeshewa katika eneo la Kamunge, Githurai. Aidha, upigaji kura ulikuwa wa mfumo wa siri.

“Uongozi tumepata, ninawaomba tupeleke GTMA mbele. Turekebishe makosa yaliyojiri kupitia viongozi wa awali, huduma za tuktuk na maruti ziwe faafu kwa kila mmoja, kuanzia wamiliki, madereva na wateja wetu,” akashauri Bw Peter Mwai, karani wa kamati teule kusimamia mipangilio na mikakati ya muungano huo.

Picha 1: Mwakilishi wa madereva wa muungano wa tuktuk na maruti Githurai (GTMA), Bw Douglas Kimani (kushoto) aliyechaguliwa. Atakuwa akisaidiwa na Bw David Mongare (aliye katikati).

You can share this post!

‘Kilimo cha miwa Mlima Kenya kina uwezo wa kuvuna...

Inter Milan wapiga Atalanta na kufungua pengo la alama sita...