HabariHabari Mseto

Madereva wote kulipa Sh5,000 kupokea mafunzo mapya

February 26th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

MADEREVA wote wa matatu, magari ya uchukuzi umma na malori ya kibiashara wanastahili kurejea darasani kwa mafunzo zaidi ya uendeshaji.

Mafunzo hayo yatakayotolewa katika taasisi tofauti za serikali yatawabidi madereva hao kulipa Sh5, 000.

Mafunzo hayo yatatolewa katika muda wa siku tano ambapo madereva 400,000 wanatarajiwa kushiriki.

Madereva hao watapewa mafunzo hayo kwa awamu katika muda wa siku hizo, na yataipa serikali Sh2 bilioni ikiwa wote watahudhuria.

Hatua hiyo ilitangazwa na serikali Januari katika hatua za kukabiliana na ongezeko la ajali za barabarani.

Kwa awamu ya kwanza, madereva 8,000 wa PSV za uchukuzi wa usiku wanatarajiwa kuhudhuria mafunzo hayo, alisema Francis Meja, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama nchini (NTSA).