Michezo

Madifenda wawili wa Gor wapigwa marufuku na CAF

January 10th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MIAMBA wa Kenya, Gor Mahia watakosa huduma za mabeki muhimu Haron Shakava na Joash Onyango dhidi ya New Star ya Cameroon jijini Nairobi hapo Januari 13, 2019.

Gor itaalika New Star uwanjani Kasarani katika mchuano wa muondoano wa kuingia mechi ya makundi ya soka ya Afrika ya Kombe la Mashirikisho.

Shakava na Onyango wameadhibiwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kwa utovu wa nidhamu katika mechi ya marudiano dhidi ya Lobi Stars ya Nigeria kwenye Klabu Bingwa Afrika mnamo Desemba 22, 2018 mjini Enugu.

Refa Tinyiko Hlungwani kutoka Afrika Kusini, ambaye alisimamia mechi hiyo, aliandika katika ripoti yake kwamba wachezaji sita wa Gor – Samuel Onyango, Jacques Tuyisenge, Joash Onyango, Haron Shakava, Mustafa Francis na Humphrey Mieno – walikosa nidhamu na akawaonyesha kadi ya njano.

Nahodha Shakava na Joash Onyango wamepigwa marufuku kushiriki mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya New Star kwa sababu katika tukio lingine Shakava alilipiza kisasi kwa kupiga teke kipa wa Lobi Stars, Kipa huyo John Eshua Lawrence alikuwa amempiga kofi.

Naye Joash aliadhibiwa kwa sababu ya “kutusi” refa baada ya kipenga cha mwisho kulia. Inasemekana Hlungwani alikuwa anajiandaa kuwalisha kadi nyekundu Shakava na Eshua, lakini kabla ya kufanya hivyo maafisa wa polisi waliondoa marefa uwanjani mashabiki walipoingia uwanjani.

Lobi Stars haijachukuliwa hatua. Kamati ya nidhamu ya CAF itakutana Januari 13 ambapo kesi dhidi ya Shakava na Joash itaamuliwa.

Uamuzi wa kesi hiyo huenda pia ukaathiri ushiriki wa mabeki hawa wawili katika mechi ya marudiano dhidi ya New Star mjini Limbe mnamo Januari 20. Mshindi wa mechi hii baada ya mikondo miwili ataingia mechi za makundi za Kombe la Mashirikisho ambalo droo yake itafanywa Januari 21.