Bambika

Madijei wanawake wanaowatoa wanaume jasho katika kucheza santuri

February 11th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KUMEKUWA na dhana kwamba tasnia ya burudani, hasa utumbuizaji, hudhibitiwa na wanaume.

Ni nadra sana kuwakuta wanawake wanaowatumbuiza watu kwenye vilabu na maeneo mengine ya burudani wakihudumu kama madijei.

Wengi huamini kuwa kazi hizo zinaweza kufanywa tu na wanaume, hivyo huwa wanaziita “kazi za wanaume”.

Hata hivyo, kuna wanawake kadhaa walioenda kinyume na dhana hizo, wakiibukia kuwa madijei sogora, wanaowika kote kote kutokana na weledi wao katika uchezaji nyimbo.

Baadhi ya wanawake hao ni DJ Pierra Makena, DJ Sonnie M, DJ Kezz kati ya wengine wengi.

Kwa wafuatiliaji wa burudani, DJ Pierra si mgeni sana. Amekuwa kwenye tania hiyo kwa zaidi ya miaka miaka 20.

Alizaliwa katika Kaunti ya Meru mnamo Aprili 11, 1981. Alisomea katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Chogoria, ambapo baadaye alielekea katika Chuo cha Mafunzo ya Uanahabari (KIMC), jijini Nairobi, kusomea masuala ya utayarishaji vipindi katika redio.

Kabla ya kuanza kazi ya udijei, alihudumu kama mwigizaji. Aliigiza kwenye vipindi vilivyopeperushwa kwenye runinga kama vile ‘Kisulisuli’, ‘Tausi’, ‘Tahidi High’ na ‘Changes’.

Alifanya kazi kama ripota katika Shirika la Utangazaji Kenya (KBC). Pia, alifanya kazi ya utangazaji katika vituo vya redio kama Radio Waumini na Hot 96 (wakati huo ikiitwa Y FM).

Alianza kazi ya udijei mnamo 2010 hadi sasa.

Ni mmoja wa madijei wanawake wanaopendelewa sana na wanaolipwa pesa nyingi zaidi kwenye hafla wanazoshiriki.

Kando na Kenya, ametumbuiza mashabiki wake katika mataifa kama Burundi, Ghana, Nigeria na Amerika.

Ndiye mwanzilishi wa tamasha la burudani la Park and Chill, ambalo hufanyika katika mataifa tofauti barani Afrika.

Anasema kuwa “bado yuko kwenye gemu”.

“Sijachoka na sitoki hivi karibuni,” asema.

DJ Sonnie M, naye ameibukia kuwa miongoni mwa madijei wachache wanawake katika ukanda wa Mlima Kenya wanaocheza nyimbo za ‘mugithi’ (mtindo wa burudani kwa lugha ya Gikuyu).

Jina lake halisi ni Muthoni Maina, na alizaliwa katika Kaunti ya Nakuru.

Safari yake ilianza mnamo 2020, alipokuja jijini Nairobi kwa mwaliko wa mcheshi Muthee Kiengei wa Watoria. Alikuwa sehemu ya wafanyakazi wa mcheshi huyo kwenye kampuni yake ya Kiengei Live.

Alitumia jukwaa na umaarufu mkubwa wa mcheshi huyo kujijenga.

Hadi sasa, amebaki kuwa dijei wa kipekee mwanamke, ambaye amekuwa akipata mialiko kwenye hafla kubwa kubwa katika ukanda huo kuwatumbuiza watu.

Kama DJ Sonnie M, DJ Kezz alipata umaarufu mkubwa wakati wa janga la Covid-19. Jina lake halisi ni Keziah Jerono Rachel na alizaliwa katika eneo la Kapsowar, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Hapo awali, alikuwa akicheza nyimbo za kidunia, lakini akaokoka na kuanza kuwa dijei wa nyimbo za injili.

Cha kushangaza ni kuwa, baada ya kuanza kucheza nyimbo za injili, alianza kutunga nyimbo.

Kufikia sasa, anaorodheshwa kuwa miongoni mwa wanamuziki wa injili wanaochipukia kwa kasi sana, hasa baada ya kutoa nyimbo kwa ushirikiano na wanamuziki kama Benachi na Rose Muhando.

Nyimbo hizo ni ‘Kilele’ (aliomshirikisha Benachi) na ‘Badilika’ aliomshirikisha Rose Muhando.

Kwenye mahojiano, alisema kuwa “huu ndio mwanzo tu wa safari yake”.